Walimu katika kaunti ya Nyamira wakiandamana barabara ya Nyamira- Kisii. Picha/HENRY NYARORA
Na CHARLES WASONGA
TUME ya kitaifa ya kutetea haki za kibinadamu (KNCHR) inawataka walimu warejee kazini, ikisema mgomo wao unawanyima watoto haki ya kupata elimu kama ilivyoangaziwa katika kifungu 53 cha Katiba.
Kaimu mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa
ya Haki za Kibinadamu (KNHRC) Bi Anne Kyalo hata hivyo alisema tume
hiyo inaunga mkono matakwa ya walimu hao ya kutaka walipwe nyongeza ya
marupurupu kulingana na mkataba kati yao na Serikali mnamo 1997.
“Japo tunaunga mkono matakwa ya
walimu, tunaunga mkono matakwa yao kwani mkataba wao uliafikiwa kwa
mujibu wa sheria. Lakini tunawaomba kurejea kazini huku viongozi wao
walijadiliana na Serikali kuhusu njia za kutanzua mzozo huo ili watoto
wasiendelee kuathirika kimasomo,” akasema Bi Kyalo.
Hata hivyo, tume hiyo iliiakshifu
Serikali kwa kutisha kutowalipa takriban walimu 240,000 wanaogoma
mishahara yao ya mwezi Juni, ikisema hiyo ni dhuluma na ukiukaji wa haki
za walimu hao. “Tunapinga vitisho kama hivi dhidi ya walimu kwani hii
ni kinyume na haki zao kama ilivyofafanuliwa katika kipengee cha 41
ibara ya 2 (c) na (d) cha Katiba,” akaongeza kamishna huyo.
Wakati huo huo, tume hiyo alipinga
mradi wa Serikali wa kutoa tarakilishi ndogo (Laptops) kwa wanafunzi wa
darasa la kwanza kuanzia hapo mwakani ikisema kuwa, Serikali
ingeshughulikia changamoto zinazokabili shule za msingi kwanza.
“Ingawa wazo hilo ni bora, hasa
ikizingatiwa kuwa hii ni enzi ya teknolojia ya mawasiliano, shule nyingi
nchini hazina walimu wa kutosha vifaa vya masomo na hata madarasa. Haya
ndio mahitaji ambayo Serikali ingepania kushughulikia wala sio
tarakilishi ambayo itaigharimu Serikali pesa nyingi, “ akasema Afisa
Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Bi Patricia Nyaundi.
Alipendekeza kuwa masomo ya kompyuta
yafunzwe wanafunzi kuanzia kiwango cha darasa la nne na wala sio darasa
la kwanza kutokana na changamoto za kutoa mafunzo hayo. “Nakumbuka
katika miaka ya zamani, ni wanafunzi wa darasa la nne kwenda juu ndio
walikuwa wakiagizwa kutumia kalamu ya wino.
Wale wa darasa la kwanza hadi tatu
walikuwa wakitumia penseli, “ akasema huku akipendekeza mfumo kama huo
utumiwe kuanzisha masomo ya tarakilishi katika shule za msingi za umma.
Tume hiyo ilibashiri kuwa huenda
uagizaji wa tarakilishi hizo ukakumbwa na kashfa kama ilivyoshuhudiwa
mwaka jana wakati wa uagizaji wa vifaa vya kusajili wapiga kura
kielektroniki (BVR) ambayo sasa inachunguzwa na Tume ya Maadili na Vita
dhidi ya Ufisadi (EACC)