Bw Aden Duale akihutubia wanahabari awali
Na ISAAC ONGIRI
WANAHABARI zaidi ya 30 nchini Kenya leo wamezua kioja katika majengo ya Bunge walipokataa kuchukua taarifa ya Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale.
Wanahabari
hao ambao walikuwa wamekusanyika bungeni walikataa kuripoti kuhusu
mkutano huo wakipinga kutimuliwa kwao katika chumba kilichotengewa
wanahabari katika majengo hayo miezi kadha iliyopita na wasimamizi.
Bw Duale na
wabunge zaidi ya 15 wa muungano wa Jubilee walikuwa tayari wameketi
katika chumba hicho kinachotambuliwa kama cha wanahabari bungeni, huku
wakiwasubiri wanahabari hao kupanga vifaa vyao, lakini walipata mshtuko
wanahabari hao walipokataa kuingia mahali hapo.
Mbunge huyo
wa Garissa Mjini na mwenzake wa Othaya Mary Wambui walitoka nje
kuwasihi wanahabari kuchukua taarifa yao lakini hawakufua dafu.
“Tumeomba mje
mchukue taarifa yetu. Tumekusanyika hapa na mimi ndio nimewaita kwa
hivyo, tafadhalini ingieni mchukue taarifa,” alisema Bw Duale. Lakini
wanahabari hao walisisitiza kuwa wanaweza tu kuchukua taarifa ya Bw
Duale na wenzake nje ya majengo hayo ili kufuata agizo lililotolewa na
Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi.
“Agizo la
Spika kuzuia kufikia chumba cha wanahabari bado halijaondolewa. Ikiwa
hilo limefanyika basi mawasiliano rasmi bado hayajafanyika. Tafadhali,
huenda ikaonekana kana kwamba tunaingia bila idhini kwa sisi kuendesha
shughuli katika kituo cha wanahabari,” mmoja wa wanahabari alimueleza Bw
Duale.
Bi Wambui aliomba suala hilo linalozua utata kati ya umma na bunge litatuliwe kwa haraka.
Ulinzi
“Hili ni suala rahisi. Linastahili kutatuliwa haraka iwezekanavyo lakini kwa sasa njoni mchukue taarifa yetu,” alisema.
Baadaye,
kundi lingine la wabunge 11 wa jamii ya Maa likiongozwa na mbunge wa
Kajiado Magharibi Moses Ole Sakuda pia walikusanyika mahali papo hapo na
kuwauliza wanahabari wachukue taarifa yao. Lakini wanahabari hao pia
walimuuliza Bw Sakuda na wenzake kuwahutubia wakiwa nje ya majengo ya
bunge wakitoa sababu zile zile.
“La, hatuwezi
kuwahutubia kutoka nje ya bunge kwa sababu baadhi ya masuala tulitaka
kujadili ni mazito na yanahitaji ulinzi wa bunge,” alisema Bw Sakuda.
Miezi miwili
iliyopita Spika wa Bunge aliagiza kituo hicho cha wanahabari kifungwe na
kompyuta zilizokuwa hapo ndani kuondolewa ili vyumba hivyo viwili
vilivyokuwa awali vimetengewa wanahabari, viweze kutumiwa sasa na kamati
za bunge.