SOKO LA LUPILA LAKITHIRI KWA UCHAFU WA CHOO

 Muonekano wa Choo cha soko la Lupila kwa nje.
 Muonekano wa choo cha soko la Lupila kwa ndani.


Wafanya biashara na wateja waliokuwa mnadani katika kata ya Lupila wilayani Makete mkoani Njombe hii leo wamelalamikia uchafu wa vyoo vya soko hilo, uliosababisha kero kwao huku wengine wakikwepa kwenda kujisaidia kwenye vyoo hivyo

Wakizungumza na mtandao huu mnadani hapo wamesema hali hiyo imekuwa tofauti na sehemu nyingine walizotembelea wilayani hapa na kufanya minada ambapo wanakuta vyoo vikiwa katika hali ya usafi, lakini waliyokutana nayo mnadani hapo hii leo ni hatari

Mmoja ya mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la Bi. Nesfaneti Digati amesema wahusika hawajajipanga vizuri katika hali ya usafi wa vyoo na hali hiyo inaonesha si kwamba imetokea leo tu bali vyoo hivyo havifanyiwi usafi kwa muda mrefu

“Tunajua Makete kwenye sehemu zote tulizopitia vyoo vinakuwa safi, mfano Ikonda, Makete na hata Kidope lakini hapa leo tumefika kwa mara ya kwanza kufanya mnada lakini hii ya leo hairidhishi kabisa” alisema Bi. Digati

Kwa upande wake Beni Sanga amesema anashangazwa na hali hiyo ya uchafu wa vyoo mnadani Lupila, na kusema endapo hali hiyo haitafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo upo uwezekano wa kuwepo magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu

Mtandao huu umefika kujionea hali ya vyoo hivyo na kuvikuta vikiwe vimekithiri uchafu, huku wengine wakijiendea vichakani kujisaidia kutokana na hali mbaya ya vyoo hivyo

Akizungumzia hali hiyo Afisa mtendaji wa kata ya Lupila Bw. Antony Solomoni Seso amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema walikuwa wamepanga kufanya kikao na halmashauri ya kijiji kuona namna ya uendeshaji wa vyoo hivyo lakini haikuwezekana kutokana na mjumbe wa halmashauri ya kijiji kufariki siku ya kikao hivyo kuahirisha

Amesema wakiwa kwenye utaratibu wa kufanya kikao kingine ndipo wakapata taarifa za mnada huo kabla ya kulifanya hilo, lakini ameongeza kuwa watakaa mara moja kulitatua suala hilo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo