Na Jennifer
Chamila,MAELEZO.
Msajili wa vyama vya
Siasa nchini amewaasa wanachama na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia
maendeleo ya nchi badala ya kutumia uwezo na muda wao kubuni mambo yanayoleta
mtafaruku na kuhatarisha amani ya nchi.
Pia amepinga tamko la chama
hicho la kuanzisha mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.Kwa mujibu wa taarifa kwa
vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini
Dar es Salaam na kusainiwa kwa niaba ya Msajili wa vyama vya siasa Sisty
Nyahoza alisema kuwa hajawahi kuruhusu
CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakamavu au mafunzo ya
kutumia nguvu ya aina yoyote kwa wanachama
wake au mtu yeyote yule.
Anaongeza kuwa CHADEMA
wanaruhusiwa kuanzisha vikundi vya kujilinda lakini hawaruhusiwi kuanzisha
mafunzo ya kutumia nguvu kwaajili ya kujilinda kama walivyo tangaza katika
mikutano yao ya hadhara kwani ni kinyume na Demokrasia na Katiba ya Jamuhuri ya
Muungano.
Nyahozo ametoa ufafanuzi
kuhusu vikundi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika Katiba ya Vyama vya Siasa
kwamba vikundi hivyo haviruhusiwi kufanya mafunzo ya kutumia nguvu ya aina
yoyote katika kutekeleza majukumu yao.Bali wajibu wao ni
kutoa taarifa wa vyombo vya Dola pale wanapo sikia au kuona uhalifu ukitokea na
wala sio kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kama tamko la
CHADEMA la tarehe 9 mwezi huu linavyo
sema.
“Hakuna maelezo yoyote katika
Katiba ya CHADEMA yanayoruhusu kutumia nguvu kufanikisha shughuli za kulinda
mali na Viongozi wa Chama.Ni vyema wananchi wote waelewe kuwa Sheria za Nchi
zimeweka masharti maalumu kwa Vyama Vya Siasa kutokana na umuhimu wa vyama hivi
katika kudumisha aman utulivu na umoja wa Kitaifa”, alisema Nyahoza.
Alisema kuwa kutokana
na Ibara ya20(2)C ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997
inasema kuwa “Bila kujali masharti ya ibara ya (1) na (4),haitakuwa halali kwa
chama chochote cha siasa kuandikishwa ambapo kutokana na katiba au sera yake:-kinakubali
au kunapigani matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake
ya kisiasa.
Nyahoza alimaliza kwa
kuwataka CHADEMA kuacha kutekeleza mpango walio tangaza wa kuanzisha makambi ya
kufanya mafunzo ya kujilinda kwa vijana wao nchi nzima,kwani kufanya hivyo ni
kukiuka sheria za nchi na endapo watashindwa kutii agizo hilo hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.