Agizo alilolitoa mkuu wa wilaya ya Makete Mh Josephine Matiro kwa afisa mtendaji wa kata ya Iwawa la kufuatilia kero ya ukosefu wa maji katika kijiji cha Ndulamo wilayani Makete mkoani Njombe, limeanza kutekelezwa kufuatia uongozi wa kata kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji hicho kujua kulikoni
Mkutano huo uliofanyika leo Jumatatu katika ofisi za kijiji hicho umewahisisha Diwani wa kata ya Iwawa Mh Benjamin Mahenge, afisa mtendaji wa kata ya Iwawa Festo Msigwa, meneja wa mamlaka ya maji Makete mjini Yonas Ndomba, viongozi wa kijiji cha Ndulamo pamoja na wananchi
Mkutano huo ulioanza saa saba mchana baada ya sintofahamu ya hati hati ya kuwepo ama kutokuwepo kwa mkutano huo, ulitawaliwa na michango yenye uchungu kutoka kwa wananchi hao ambao wanadai wamechangia fedha nyingi kutoka mifukoni mwao pamoja na kuuza msitu wa kijiji kwa ajili ya mradi wa maji katika kijiji chao lakini hadi sasa maji hawapati
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, meneja wa mamlaka ya maji Makete mjini Bw. Yonas Ndomba amesema mapendekezo yaliyotolewa na yeye katika hatua za awali za kuanza kwa mradi huo, alipendekeza mabomba ya daraja B, C na D ndiyo yanunuliwe kwa ajili ya mradi huo, lakini katika utekelezaji yalinunuliwa mabomba ya daraja B na C tu ambapo katika ufungaji kuna maeneoambayo mabomba hayo hayakuweza kuhimili na ndipo baadhi ya mabomba yalipasuka na kuvujisha maji
Amesema ingawa tatizo hilo limejitokeza lakini kwa hivi sasa mamlaka yake imeshapeleka maombi ya fedha wizarani tangu mwezi Aprili mwaka huu kwa ajili ya maboresho ya maji Makete mjini ikiwemo na kijiji cha Ndulamo ambapo fedha hizo zikitoka zitarekebisha tatizo hilo la maji katika kijiji hicho na kubaki historia
Ndomba amesema kwa hivi sasa kwa kuwa tatizo linaeleweka limesababishwa na nini hakuna sababu ya kurushiana mpira na badala yake kujadiliana kwa pamoja ili ufumbuzi wa tatizo hilo upatikane na wananchi hao wapate maji, ambapo alisema anatarajia mwishoni mwa mwezi huu fedha kutoka wizarani zitafika na utekelezaji utaanza mara moja
Mmoja wa mkazi wa kijiji hicho Bi Zaida Mahenge amelaani kitendo kilichofanywa na wataalamu wa idara ya maji kuwaambia kuwa mabomba hayo yanafaa kwa ajili ya matumizi ya mradi huo ilihali hayawezi na kudai kuwa kwa kuwa wananchi hawana utaalamu huo ni vyema wataalamu wakaona huruma jinsi wananchi wanavyotoa fedha kwa ajili ya michango ya mradi huo, na kama wangewaambia ukweli tangu mwanzo wananchi hao wangeona cha kufanya, huku Bw. Samora Chaula akiwataka wananchi hao kutoa mabomba hayo yaliyochanika baada ya kufungwa na wao kuyafungua na kuyahifadi stoo kuyatoa na kuwapa viongozi hao wa kata waondoke nayo kwa kuwa hayana msaada kwao
"Wananchi wa Ndulamo tayari tumeshaumia kuhusu maji, sasa sisi tunayalinda tu bure hapa haya mabomba ambayo ni mabovu hapa, tuyatoe na tuwakabidhi viongozi hawa wa kata waondoke nayo sisi hatuyataki" alisema Chaula
Hali hiyo ilijibiwa na meneja wa maji Bw. Ndomba kuwa madaraja ya mabomba ya maji yanatofautiana na kuwa mabomba hayo wanayoyaona kuwa hayafai lakini yatakuja kupata kazi kubwa baadaye ikiwemo hatua ya usambazaji kwenda kwenye nyumba za watu hivyo wazidi kuyatunza
Akiwatoa hofu wakazi hao kuhusu kumalizika kwa tatizo la maji Ndulamo mtendaji wa kata ya Iwawa Bw. Festo Msigwa amewataka wananchi hao kuwa na subira kidogo ya kusubiri fedha hiyo kutoka wizarani, na kuahidi kufuatilia bega kwa bega utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike mapema kama walivyokubaliana na kuomba ushirikiano kwa wananchi kuhusu hilo, na kusema hayo yaliyoamuliwa kwenye kikao cha leo atayawasilisha kwa maandishi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Makete
Wakati wakisubiria fedha kutoka wizarani, mkutano huo ulikubaliana kwa pamoja meneja wa maji Makete mjini kesho Jumanne kwenda kupima upya eneo mambomba yalipopasuka hadi kwenye tanki kuona ni mambomba kiasi gani yatahitajika ili yatafutwe kwa haraka yaunganishwe na maji yatoke angalau yafike shule ya msingi Ndulamo ambayo ina wanafunzi zaidi ya 700!