KILI YAIKABIDHI SIMBA SC MILIONI 20 KWA AJILI YA MKUTANO MKUU

Meneja wa Kili, George Kavishe akimkabidhi Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa wanachama wa klabu hiyo utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia katikati ni Geoffrey Makau, Msaidizi wa Meneja wa Kili. Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam leo. (Picha: Executive Solutions)

Kili leo imekabidhi hundi ya Sh. Milioni 20 kwa klabu ya Simba SC kwa ajili ya mkutano mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Julai 20, 2013 jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi hundi hiyo Meneja wa Kili, George Kavishe alisema: “Tunakabidhi fedha hizi ikiwa ni mwendelezo kutekeleza majukumu yetu kama mdhamini mkuu wa Simba SC. Kwa kuzingatia hilo tungependa kuona maendeleo ya klabu ya Simba uwanjani na nje ya uwanja. 

Tunaiunga mkono klabu hii katika mkutano wake mkuu tukiamini kuwa mkutano huu utaimarisha uhusiano uliopo kati ya klabu na wanachama wake kwa kuwapa fursa ya kuhakiki mwelekeo wa klabu yao waipendayo.

Kavishe alieleza zaidi, “Ikiwa na mamilioni ya mashabiki nchini, klabu hii imejengeka kutokana na rekodi nzuri ya mafanikio kwa muda mrefu – na Kili inajivunia kuwa sehemu ya klabu hii. 

Tunaamini kwamba mbali na wanachama, wapenzi na mashabiki wa Simba kuona timu yao ikishinda lakini pia tunatambua kwamba ni haki yao ya msingi kuwasiliana na klabu na kupata taarifa mbalimbali za mwenendo wa klabu.

Kutokana na sababu hizi, sisi kama wadhamini wakuu wa klabu hii tunatoa mchango wa shilingi milioni ishirini ili kuunga mkono jitihada za klabu kuendelea kuwajibika kwa wanachama wake.

“Tunatambua wajibu wetu kama wadhamini wakuu wa Simba katika kutekeleza mkataba wetu, tutaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha tunalipeleka soka la Tanzania kwenye kilele cha mafanikio."


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo