ZAIDI YA SH. MILIONI NNE ZINAHITAJIKA KUTATUA TATIZO LA MNARA ZBC


003
Miza Othman na Mwanaisha Muhammed,  Maelezo-Zanzibar

ZAIDI ya shilingi milioni nne zinahitajika kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi tatizo la kuharibika kwa mnara wa kurushia matangazo ya masafa ya kati katika redio ya Shirika la Utangazaji Zanzibar ulioko Bungi Wilaya ya Kati Unguja.

Hayo yameelezwa na Fundi Mkuu wa ZBC Redio Ali Aboud Talib, mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, alipofanya ziara huko Bungi kuona uharibifu uliosababisha kukosekana
  kwa matangazo hayo kwa mwezi mzima sasa.

Aboud amesema hali hiyo imetokana na kuharibika kwa kifaa cha kebo ya frikwensi, kinachotumika kusambazia matangazo  ya redio ya ZBC kwa masafa ya kati.

Mapema, Waziri Mbarouk amelitaka Shirika la Utangazaji Zanzibar kufanya jitihada za haraka kulipatia ufumbuzi wa haraka tatizo hilo, ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wa Zanzibar ambao hutegemea zaidi
redio hiyo.

Amesema lengo la serikali ni kuona wananchi wake wanapata matangazo ya redio yao ya taifa kwa siku na muda wote na kwa karibu zaidi.
 
Kwa hivyo, amewataka watendaji wa shirika hilo kujipanga na kuhakikisha tatizo hilo linarekebishwa kwa hali na mali na kama likishindikana nguvu za ziada zitatumika ili kurejesha matangazo ya
masafa ya kati.

Waziri huyo pia amesisitiza kuwepo ushirikiano kati ya wafanyakazi wa shirika hilo ili kunapotokea tatizo liweze kutatuliwa ipasavyo.
 
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR 7/6/2013


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo