WAKATI mwingine ndugu zangu wadau hakuna ambaye
hafurahii kukua kwa teknolojia hasa ya upashanaji habari kwa njia
mbalimbali ambazo zitamsaidia mtu kufahamu matukio anuai ambayo kimsingi
yatamtoa hapo alipo ki-taarifa na kuhabarika zaidi.
Lakini hali hii ya kukua kwa kasi imekumbwa na maudhi ambayo nina
hakika si mimi peke yangu nimeyaona ila wapo waliotangulia na wakasema,
lakini pia imefika zamu yangu kusema na nina imani kuwa hata wenzangu
wanakumbana nayo ipo siku nao watasema.
Ongezeko la mitandao tando (blogs) hakuna asiyejua kuwa ni msaada
mkubwa wa kuwafikishia watu habari kama utatimiza malengo yako kwa kuwa
ulipokuwa na mpango wa kufungua hiyo blog yako lazima ulikuwa na malengo
ambayo bila shaka ulikaa chini na kuona kuwa utayamudu.
Nichukulie mfano kwa nchi yetu ambayo ni kubwa, si kila habari
unaweza kuipata kwa kufika eneo la tukio na ukaichukua kutoka kwenye
vyanzo husika, labda uwe na waandishi wa habari katika mikoa ama wilaya
zote za Tanzania, lakini kwa kuwa wamiliki wengi wa mitandao tando
(blogs) hawana uwezo huo, inawalazimu kuchukua habari ambazo tayari
zimewekwa kwenye mitandao ya mwanalibeneke mwenzako na kuziingiza kwenye
blogs zao, kwa maana nyingine tunategemeana.
Hili si tatizo bali nachoona mimi kuwa ni tatizo ni kuwa baadhi ya
wanalibeneke(bloggers) wengi wanakosea hata “kucopy” na “kupaste” jambo
ambalo limekuwa likiboa wasomaji wa blog zetu kwa kuwa unaweza kukuta
habari moja imekosewa kwenye zaidi ya blog 50 ambazo zimeweka habari
hiyo hiyo, jambo linaloshiria kuwa mtu ana copy habari na kuipaste kwake
bila hata yeye mwenyewe kuisoma, sasa kama wewe huisomi na kuihariri je
unataka nani aisome na kuirekebisha?
Na si hilo tu, pia si kila habari iliyopo kwenye blog ya mwenzako
inatakiwa iwepo kwenye blog yako kwa kuwa kama ndiyo hivyo je ni kwa
nini kusiwe na blog moja itakayokuwa na habari zote, kwa kuwa unakuta
habari zilizoko kwenye blog moja ndiyo hizo hizo zipo katika blog zaidi
ya 20 sasa unajiuliza tofauti za blog zetu kwa sasa ni majina ama ni
nini? Ninaposema si kila habari lazima iwe kwenye blog yako namaanisha
zipo habari ambazo mmiliki wa mtandao kazitafuta angalau kutofautisha
blog yake na nyingine, mfano kakuta mifugo inazurura mitaani akaipiga
picha na kuziweka kwenye blog yake, unakuta wamezinakili na kuziweka
kwao, tena wakati mwingine bila hatimiliki ya mwenye picha ama
ulipoinakili, sasa unajuuliza hivi wamiliki hawa hawajui kutofautisha
habari za “kucopy” na za kuacha?
Huu si muda wa kuwaudhi wasomaji kwa kukuona kuwa huna ubunifu na
namna ya kuelewa ni jinsi gani ya kunakili habari na habari ipi uiache,
mfano rais akiwa na ziara sehemu fulani mathalani hapa nchini, lile ni
tukio ambalo linatazamwa na nchi nzima kufahamu kinachoendelea na
wanahabari wanaokuwa naye ndiyo tunaowategemea kwa habari za ziara hiyo,
ambapo hata ukizinakili zinaleta mantiki, lakini usisahau kutoa hati
miliki ya mwenye habari.
Hebu tubadilike na tuone huu ni muda wa kutumia vizuri libeneke zetu
ili zizidi kuwavutia watu, na kama unaona huwezi, hebu jifunze kwa
wanaoweza wakuelekeze halafu uje kuendelea na kitu chenye ubora na mvuto
kwa wasomaji
Ni hayo tu wadau
Edwin Moshi
Edwin Moshi
EDDY BLOG