Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye amewatahadharisha vijana kuwa wanaelekea
kwenye uchaguzi mkuu wasikubali kupewa rushwa ya kanga, fulana na fedha
na mtu yeyote anayetaka kuingia madarakani.
Akizungumza
jana alipokuwa kwenye bonanza la michezo la kikundi cha Ukwamani Jogging
kilichopo Kawe, alisema vijana wawe makini katika kuchagua mtu mwenye
uwezo wa kuongoza ambaye atajali masilahi ya wananchi wake siyo kwa
masilahi yake binafsi.
“Najiuliza
kama ninajiamini nataka kugombea Kawe au Arusha au Sumbawanga kama
ninafaa na wananchi wananiamini mimi ninafaa na wananchi wananihitaji
kwa nini niwachochee kwa kanga au fedha ukiona hivyo huyo hawafai
kuwaongoza,” alisema na kuongeza:
“Ukiona mtu anatoa kitu ili achaguliwe hafai kuwa kiongozi kwani uongozi ni mzigo,” alisema Sumaye.
Aliwashangaa
watu wazima wanaochukua fedha na kuweka mfukoni kisha wanapita mitaani
huku wakisema fulani anafaa kwa kuwa anatoa rushwa na fulani hafai kwa
kuwa hatoi kitu chochote.
Sumaye
alisema anayetoa fedha ili apewe kura huyo hafai kuwa kiongozi kwa
sababu atakuwa anawatumikia watu wake waliompa fedha sio mwananchi
ambaye alijitolea kumchagua kiongozi hiyo kwa kumpigia kula halali ili
aweze kusaidia kumtatulia kero mbalimbali zinazomkabili.
Alisema kama
kuna watu wanaumizwa kwa kuambiwa wanapokea au kutoa rushwa huku akiwa
anaendelea na kufanya hivyo aache ili asiendelee kuumizwa na hilo.
Sumaye
alisema nchi haiwezi kuwa na maendeleo kama viongozi wataendelea
kudidimiza nchi kwa rushwa,ufisadi na kuingiza dawa za kulevya nchini.
Alisema
viongozi wanaoleta dawa za kulevya kama ni nzuri wangezitumia lakini
hawazitumii matokeo yake wanaoathirika ni vijana ambao wanategemewa
kulijenga taifa hili.
“Hatuwezi
kudidimiza jamii kwa kuwaletea dawa za kulevya ili watoto wa wenzao
waharibikiwe kwa nini wasiwape au kutumia hao viongozi ili waathirike
wao wenyewe?” alisema Sumaye.