Mahakama ya kimataifa imeamua kuwa Naibu wa rais wa Kenya ambaye pia
ni mshukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi Kenya, William Ruto, awepo
mahakamani Hague wakati kesi yake ikisikilizwa.
Hasa mahakama inamtaka Ruto kushiriki baadhi ya vikao muhimu katika
mahakama hiyo wakati kesi yake itakapokuwa ikisikilizwa kuanzia mwezi
Septemba mwaka huu.
Bwana Ruto alikuwa ameiomba mahakama imruhusu ashiriki vikao hivyo kwa njia ya video kwenye mtandao wa Internet.
Mahakama imesema kuwa imemruhsu kutohudhuria vikao vingine kutokana na majukumu ya wadhifa wake.
Aidha Ruto alikanusha madai kuwa alihusika katika ghasia za baada ya
uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 ambapo mamia waliuawa na maelfu kuachwa
bila makao baada ya kufukuzwa makwao kufuatia vita vya kikabila.
Alishtakiwa na Rais Uhuru Kenyatta . Wawili hao walikuwa mahasimu wa kisiasa wakati wa uchaguzi miaka sita iliyopita.
Watu 1,200 walifariki na wengine laki tano kuachwa bila makao katika
vita ambavyo nusura vitumbukize nchi kwa mapigano ya wenyewe kwa
wenyewe.
Mahakama ya ICC ilisema kuwa Ruto atastahili kuhudhuria ufunguzi wa
kesi yake pamoja na kikao cha mwisho ambapo wahusika wa kesi watatoa
kauli yao ya mwisho kabla ya uamuzi kutolewa.
Pia atatakiwa kuhudhuria kikao ambapo jaji watatoa uamuzi katika kesi hiyo na siku ya kutolewa kwa hukumu ikiwa.
Mapema mwezi huu majaji katika mahakama ya ICC, walikubali ombi la
mawakili wa Ruto, kuakhirisha tarehe ya kuanza kwa kesi dhidi yake ili
wapate muda zaidi kujiandaa.
Mahakama pia imependekeza baadhi ya vikao vya kesi kusikilizwa nchini Kenya au Tanzania.
Tangazo lilijitokeza wiki chache baada ya shinikizo kutoka kwa
mataifa mengine ya kiafrika kuitaka mahakama kufutilia mbali kesi dhidi
ya Kenyatta na naibu wake Ruto.
Muungano wa Afrika ulisema kuwa mahakama hiyo ina ubaguzi , tuhuma
ambazo mwendesha mkuu wa mashtaka katika mahakama hiyo alikanusha
vikali.
Kesi dhidi ya rais Kenyatta inatarajiwa kuanza mwezi Julai.
Chanzo: bbcswahili