MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Iganduka wilayani Mbozi Mkoani Mbeya
Makrina Simbowe (42) anashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani hapa kwa
kosa la kumuua mumewe aitwaye Rodrick Mwaipasi (55) baada ya mwanamke
huyo kuuza karanga debe mbili bila idhini ya mume wake.
Tukio la kifo cha mwanaume huyo linatokana na marehemu kuhoji kwa mke
wake juu ya kuuza karanga debe mbili bila idhini yake na hivyo mwanamke
huyo kumsukuma mume wake ambaye aliangukia kisogo na kufariki papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi
Mkoani Mbeya Bw.Diwani Athuman alisema tukio hilo limetokea juni 24
mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika kijiji cha Iganduka wilayani
hapa
Baada ya marehemu kusukumwa alidondoka na kupelekwa katika hospitali
mbozi mission ambapo hata hivyo alikuwa ameshafariki kutokana na
kuangukia kisogo.
Aidha Diwani alisema chanzo cha mzozo huo ugomvi wa kifamilia uliotokea
kati yao kisha marehemu kusukumwa na mke wake na kufariki dunia.
Hata hivyo Kamanda Athuman alisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na
taratibu zinafanywa ili afikishwe mahakamani ,na kutoa wito kwa jamii
kutatua matatizo/migogoro yao kwa njia ya mazungumzo badala ya
kujichukulia sheria mkononi kwa kutumia hasira na nguvu.