Vijana wenzangu na wote wenye dhamira ya kuwezesha maendeleo ya vijana nchini, salaam!
Mtakumbuka kwamba mwezi Januari 2013
nilitoa taarifa kwa umma ya kueleza kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa
Bunge Muswada Binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa na kuomba
hatua za ziada toka ofisi ya Bunge kwa kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni
ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Toka wakati huo muswada huo mpaka sasa
Mei 2013 haujachapwa katika gazeti la Serikali na nimepokea barua toka
kwa ofisi ya Bunge kwamba wamepokea ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kuwa muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali
kwa kuwa umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi.
Sababu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kutoa ushauri huo ni kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine
kupitia kifungu cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la vijana la
taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya
maendeleo ya vijana.
Kwa maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ametoa ushauri huo bila kuzingatia kwamba kifungu cha 31
kipengele cha pili kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo
kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali
na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha
pili cha katiba ya Nchi.