ASILIMIA 26.8 hadi asilimia 31.9 ya Watanzania
wanatumia pombe na asilimia 27.4 kati ya hao ambao ni wanaume na wengine
asilimia 13.4 ambao ni wanawake, ni walevi wa kupindukia. Bunge
lilielezwa jana.
Takwimu hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid, ambaye alisema kuwa viwango hivyo vimetokana na utafiti
uliofanywa kati ya Februari hadi Oktoba mwaka jana 2012.
Alikuwa akijibu swali la Abdallah Haji Ali (Kiwani–CUF) aliyetaka
kujua kauli ya Serikali kuhusu utumiaji wa pombe ambao umethibitika kuwa
ni hatari kwa afya za binadamu. Pia alipendekeza pombe ipigwe marufuku
kabisa hapa nchini kwa kuzingatia madhara yake.
Naibu waziri alisema tafiti zimeonyesha kuwa watu milioni mbili
wanafariki dunia kila mwaka duniani kutokana na madhara ya matumizi ya
pombe na asilimia nne ya matatizo ya kiafya yanatokana na matumizi ya
pombe.
“Hali inazidi kuwa mbaya zaidi katika nchi zinazoendelea hasa
kutokana na kukabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na ustawi wa jamii
inayochangiwa na magonjwa ya malaria, kifua kikuu na Ukimwi,” alisema Dk
Rashid.
CHANZO:MWANANCHI