Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akishuhudia
misumeno ya moto 23 katika eneo la Kizimbani Pemba, ambayo imekusanywa
kwa ajili ya kuchomwa moto, ikiwa ni kampeni ya kutokomeza misumeno hiyo
Zanzibar
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo na
Maliasili, Mtumwa Kheir Mbarak akizungumza katika hafla ya uchomaji moto
wa misumeno ya moto 23 katika eneo la Kizimbani Pemba.
Mtumiaji
wa nishati mbadala itokanayo na kinyesi cha ng’ombe Hamad Juma Hassan,
akitoa maelezo mbele ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuhusiana na
utengenezaji wa nishati hiyo, wakati Maalim Seif alipomtembelea nyumbani
kwake Kinyasini Pemba.
Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim, akimueleza
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kuhusiana na maendeleo
ya kilimo cha mpunga wa majaribio kisiwani Pemba.Picha na Salmin Said-Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
--
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka
wananchi kushirikiana kuisaka misumeno ya moto popote ilipo ili iweze
kutokomezwa kabisa katika visiwa vya Unguja na Pemba.Ameeleza
hayo katika kampeni maalum ya kutokomeza misumeno ya moto ambapo
misumeno 23 imechomwa moto mbele ya kiongozi huyo, baada ya kukamatwa na
maofisa wa Idara ya misitu.
Amesema
kila mtu ana wajibu wa kushirikiana na jamii katika kufichua misumeno
iliyobakia, ili kuhakikisha kuwa haitumiki tena na kusababisha athari za
kimazingira.
“Kila
mtu ana wajibu wa kuwafichua watumiaji wa misumeno hii, lakini mashena
na polisi jamii muna jukumu kubwa zaidi, na nina hakika mukiamua
munaweza kuwabaini wote wenye misumeno ya moto”, alisema Maalim Seif.Amesema
iwapo misumeno hiyo haitodhibitiwa inaweza kuiathiri nchi kwa kiasi
kikubwa kutokana na uwezo wake wa kukata miti kwa muda mfupi.
Uchomaji huo wa misumeno ya moto 23 umefanyika katika ofisi za Idara ya misitu iliyoko Kizimbani Kisiwani Pemba.Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya kilimo na maliasili Affan Othman
Maalim amesema misumeno ya moto ipatayo 270 bado inakisiwa kuwepo
Zanzibar, na kwamba kampeni hiyo itasaidia kuitokomeza.
Kwa
mujibu wa Affan, kisiwa cha Pemba kinaongoza kwa kuwa na misumeno mingi
ya aina hiyo ipatayo 150, huku Unguja kukiwa na misumeno zaidi ya 120.Amefahamisha
kuwa takriban ekari 1000 za miti hupotea kila mwaka visiwani Zanzibar
kutokana na kukatwa ovyo na kuongezeka kwa kasi hiyo kutokana na
matumizi ya misumeno ya moto.
Naibu
Waziri wa Kilimo na Maliasili Mtumwa Kheir Mbarak, amesema misumeno
hiyo ambayo ni adui wa muda mrefu wa mazingira, inaweza kuiweza kuifanya
nchi kuwa jangwa kwa muda mfupi na ni hatari pia kwa afya ya binadamu.
Maalim
Seif yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambako
anatembelea shughuli za kilimo kwa lengo la kuwahamasisha wakulima
kuendeleza kilimo chenye tija kwa kutumia utaalamu wa kisasa na mbegu
bora.
Katika
Mkoa wa Kaskazini Pemba ambako alianza ziara yake alitembelea shamba la
utafiti wa uzalishaji wa mpunga wa mbegu ya nerika liloko Gombeume
mchangamdogo, skuli ya wakulima iliyoko Kiongweni Kambini, shamba la
viazi vitamu Makangale na skuli ya wakulima juu ya nishati mbadala
iliyoko Kinyasini.
Na
Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar