KIZAAZAA CWT MAKETE

Mwenyekiti wa CWT Makete Mwl. Lutangilo Sanga (kulia) akizungumza na mwandishi wa habari hii

Ikiwa zimepita siku kadhaa sasa tangu kufanyika sikukuu ya wafanyakazi, kumeibuka sintofahamu katika chama cha waalimu(CWT) wilaya ya Makete kutokana na kuwepo tuhuma kuwa baadhi ya waalimu waliuziwa fulana zilizotolewa na chama hicho taifa kwa ajili ya kusherehekea kinyume na makubaliano

Hii inatokana kuwepo baadhi ya waalimu kudai kuwa waliuziwa fulana hizo kwa shilingi 1,000/= kwa fulana moja tofauti na agizo la CWT makao makuu kuwa waalimu wote wapewe fulana za Mei mosi bure

Kutokana na minung’uniko iliyokuwa ikitolewa na watu wanaosadikika kuwa ni waalimu ambao hawakutaka kutaja majina yao, ripota wetu alilazimika kumfuata mwenyekiti wa chama cha waalimu wilaya ya Makete Bw. Lutangilo Sanga ambaye bila kumumunya maneno alimtwisha lawama katibu wa chama hicho wilaya ya Makete kuwa ndiye aliyepokea shilingi elfu moja moja za fulana hizo

Mwenyekiti huyo alisema amesikia tetesi hizo ambapo pia alipigiwa simu na baadhi ya waalimu ambao hakuwataja, ambao walimpa malalamiko yao kuwa wameuziwa fulana za Mei mosi licha ya kuwa na taarifa kuwa fulana hizo walitakiwa kupewa bure, jambo alilosema hakuwa na majibu nalo kwa kuwa katibu wake ndiye alikuwa akilishughulikia

Mwenyekiti huyo alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa katibu wake amekuwa akifanya baadhi ya mambo bila kumshirikisha na ndiyo maana yeye anakosa majibu, lakini alipoulizwa na mwandishi wetu kuwa kama mwnyekiti amechukua hatua gani kama katibu wake hamshirikishi, hakuwa na jibu

“Mimi nifanyeje kama hanishirikishi na ndiyo maana yanatokea kama haya” alisema 

Mtandao huu ulilazimika kumfuata Katibu wa chama cha waalimu wilaya ya Makete aliyejitaja kwa jina moja la Kapinga na kushangazwa na taarifa hizo huku akisema kuwa hajauza hata fulana moja kwa waalimu na kama wapo waalimu waliouziwa fulana wakadai fedha zao

Katibu CWT Makete
“Ndugu mwandishi wa habari orodha ya waliopokea fulana za mei mosi hizi hapa, na hawa ndio wamepokea kutoka kwangu, mimi wakati nagawa fulana nilikuwa naonana na viongozi tu, kama ni mratibu elimu, ama mwakilishi yeyote namkabidhi fulana na kofia za kata ama shule yake, anasaini naondoka, kama orodha hii( huku akiionesha) ilivyo sasa huo uuzaji unatoka wapi” alisema Kapinga

Alisema kama kuna mwalimu yeyote ambaye ameuziwa fulana na katibu huyo ajitokeze hadharani, na yuko tayari kuwajibika kwa hilo kama ni kweli yeye amewuzia waalimu fulana, huku akisema yeye kama mtendaji mkuu wa chama hajapokea malalamiko yoyote ofisini kuhusu waalimu kuuziwa fulana

Ameongeza kwa kuwa yeye alikuwa akigawa fulana hizo kiujumla kulingana na idadi ya waalimu wa shule, inawezekana wapo baadhi ya waliozipokea halafu wakaenda kuziuza kwa waalimu, ambapo kosa si lake bali ni la aliyeuza ingawa anafahamu kuwa zinapaswa kutolewa bure, na aliyefanya hivyo anapaswa kurejesha fedha za mwalimu huyo na hatua nyingine zitafuata

Kuhusu tuhuma kuwa amekuwa akijiamulia mambo bila kumshirikisha mwenyekiti wake, katibu huyo alisema si kweli na badala yake asema yeye mwenyekiti ndiye amekuwa akijiamulia mambo mwenyewe ikiwemo kuitisha vikao ilihali muitishaji wa vikao ni katibu kama katiba ya chama inavyoelekeza

“Mfano mzuri ni hii barua hapa ameitisha kikao na amesaini, bila hata kunishirikisha ilihali mimi katibu ndiye muandaaji wa vikao kwa kushirikiana na yeye, sasa yeye kawaita wajumbe kwa barua hii na kufanya kikao, sasa hapo nani hamshirikishi mwenzie” alisema Kapinga


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo