Na Frank Geofray, Jeshi la Polisi
Maofisa na askari Polisi kote
nchini wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa
suala hilo siyo la hiari bali ni la lazima kulingana na kanuni pamoja na
taratibu za ufanyaji wa kazi za Polisi.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini IGP Said Mwema, wakati wa kikao cha kikazi kilicho
wakutanisha maofisa wa Polisi Makao makuu, Kanda maalumu ya Dar es
Salaam na Vikosi vya Jeshi hilo chenye lengo la kuwajengea uwezo na
kupeana mafunzo yatakayosaidia kufanya kazi kwa weledi zaidi ili kuweza
kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa aina mpya unaojitokeza hapa nchini
katika sura mbalimbali.
Aidha, IGP Mwema alisema, kila
ofisa na askari polisi anapaswa kutekeleza kwa vitendo utoaji wa huduma
bora ndani na nje, ikiwa na maana kwa askari wenyewe na kwa wananchi,
ili kuendana na maboresho yanayoendelea ndani ya Jeshi hilo na kuweza
kukabiliana na vitendo vya vurugu na matishio mengine ya kihalifu na
wahalifu yanayojitokeza hapa nchini.
Aliwatataka Makamanda na maofisa
wa polisi wote kuendelea kuwa karibu na wananchi ili kujua kero za
kiusalama zinazowakabili na kwa pamoja kuweza kuzitafutia ufumbuzi ili
kuondoa hofu ya uhalifu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa jambo ambalo
litaendelea kuimarisha hali ya usalama hapa nchini.
Aidha Mwema, amesema Jeshi la
Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali baadhi ya watu wanaotumia
mwamvuli wa siasa au dini kama kisingizio cha kufanya ama kuchochea
vurugu hapa nchini kwa kuwa vurugu hizo ni kosa la jinai kama yalivyo
makosa mengine ya jinai.
“Hakikisheni mnawakamata wale
wote wanaofanya vitendo vya vurugu kwa visingizio vya siasa kwa kuwa
siasa zao zinaishia pale tu wanapokuwa wamefanya vitendo vya vurugu
ambavyo ni kosa la jinai na sisi hatuwezi kuwafumbia macho” Alisema
Mwema.
IGP Mwema alisema Jeshi la Polisi
litaendelea kufanya kazi zake kwa kufuata kanuni, maadili na taratibu
zinazoliongoza katika kuhakikisha amani na usalama vinadumu hapa nchini
na kusisitiza kuwa askari wa Jeshi la polisi si wanachama wa chama
chochote cha siasa japokuwa wanaruhusiwa kupiga kura.
