TAASISI YA WAMA YAKABIDHI VIFAA VYA AFYA MKOANI RUKWA


Anna Nkinda-Sumbawanga
Taaasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeikabidhi hospitali ya mkoa wa Rukwa - Sumbawanga kontena la  urefu wa futi 40 lenye mitambo ya kisasa na vifaa vya huduma ya afya ilivyochangiwa na Shirika linayoshughulika na utoaji wa huduma za kibinadamu la  Project C.U.R.E la nchini Marekani vyenye thamani  ya zaidi ya shilingi milioni mia saba .

Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika viwanja vya Hospitali hiyo ambapo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia  ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo aliwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi na si vinginevyo.

Akiongea na wananchi wa mkoa huo pamoja na wahudumu wa afya waliohudhuria hafla hiyo  Mama Kikwete alisema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo ni kutokana na changamoto mbalimbali alizokuwa  ameelezwa katika ziara zake za mikoani ambazo zilimpa  msukumo mkubwa wa kwenda mataifa mbalimbali kwa kuwa  aliona anao wajibu wa kufanyia kazi matatizo aliyoelezwa yakiwemo ya upungufu wa vifaa vya kutolea huduma za afya. 

 “Bila ya shaka yoyote vifaa na mitambo ninayoikabidhi leo vitafanya kazi kubwa katika kutoa huduma bora zaidi ya afya  na kuokoa maisha ya wananchi wetu katika hospitali ya Sumbawanga”, alisema Mama Kikwete.

Akisoma taarifa ya Hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. John Gurisha alishukuru kwa mitambo na vifaa tiba walivyopewa  na kuahidi kufanya kazi kwa uwezo wao wote ili kufanikisha azma ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dk. Gurisha  alisema kuwa hospitali hiyo inahudumia wakazi wa mkoa huo na Katavi wapatao 1,760,639  na wanatoa huduma za tiba, kinga na ushauri wa kitaalamu. Inauwezo wa kuwa na vitanda 450 na wastani wa kulaza wagonjwa 300 kwa siku  lakini kwa sasa inavitanda 270 na inalaza wagonjwa 160 kwa siku. 

“Baadhi ya changamoto tunazokabiliana nazo ni upungufu wa watumishi wenye ujuzi, ucheleweshaji wa matengenezo ya vifaa mara linapotokea tatizo na hivyo kusababisha wagonjwa kutopata huduma inayostahili kwa wakati na  imani na mila potufu katika jamii imekuwa ni kipingamizi kikubwa katika utoajia wa huduma bora za afya kwani wagonjwa wengi wamekuwa wakichelewa kufika hospitali mpaka wapitie kwanza kwa waganga wa jadi”, alisema Dk. Gurisha. 

Aliyataja mafanikio waliyoyapata kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita kuwa ni kuajiri madaktari saba na wauguzi 11, wamepata wateknolojia watano wa maabara kutoka Taasisi ya Benjamini William Mkapa, wamejenga chumba cha kuhifadhi dawa za chanjo, wodi ya wagonjwa wa akili, wodi moja ya daraja la kwanza , maabara ya kisasa kwa msaada wa Serikali ya Marekani, chumba cha upasuaji na wodi ya wazazi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Project C.U.R.E Dk. Abdul Kimario alimpongeza Mke wa Rais kwa jitihada alizozifanya kwa muda mrefu za kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vimefika nchini na kuwaomba watanzania wamuunge mkono kukabiliana na upungufu wa vifaa tiba mahospitalini kwani jitihada alizofanya ni kubwa na  amepanda mbegu ambayo itaota kwa miaka mingi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo