TAARIFA RASMI KUHUSU UPATIKANAJI WA DAWA ZA MALARIA



Utangulizi
Kumekuwepo na taarifa kupitia baadhi ya vyombo vya habari kwamba kuna upungufu mkubwa wa dawa mseto za kutibu malaria aina ya ALU katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.Taarifa hizo zilimnukuu Mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la SIKIKA, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika mjini Dar es Salaam hivi karibuni.

 Ufafanuzi
Taarifa alizotoa Mkurugenzi wa SIKIKA, chanzo chake kimetokana na kunukuu taarifa zinazopatikana kutoka katika mfumo wa kielektroniki wa wizara ambao unafuatilia takwimu za dawa za malaria katika vituo vya huduma ujulikanao kama ‘SMS for Life’.

Mfumo huu unatoa taarifa za upatikanaji wa dawa za kutibu malaria aina mbili tu ambazo ni Alu na Quinine, na sio dawa nyingine za kutibu Malaria.
 Hivyo basi, dawa zingine zote pamoja na zile za msaada, ambazo zinapokelewa na kusambazwa katika hospitali zote nchini hazitolewi taarifa kwa kutumia mfumo huu wa “SMS for Life”. Hivyo kusababisha wakati mwingine kuonekana hakuna dawa wakati dawa hizo  zipo vituoni.
 Hali halisi

 Dawa za Alu zilizopokelewa mwezi Januari 2013;-
  • Vidonge vya watoto  dozi  2,400,000 ambazo zitatosheleza kwa miezi 5
  • Vidonge vya watu wazima dozi 5,688,720 zinatosheleza matumizi ya miezi 14
 Shehena nyingine za dawa za Alu zinatarajiwa kufika nchini mwezi Machi, 2013.
 Aidha, kufikia tarehe 31 Disemba 2012 kulikuwa na dawa za Alu za watoto dozi 1,315,967 ambazo zilitosha matumizi ya miezi 2.  Vile vile, kulikuwa na dozi za Alu 2,283,610 za watu wazima ambazo zinatosha matumizi ya miezi 2 na nusu.

 Hitimisho
 Wizara inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba kwa sasa kuna dawa za kutibu malaria vituoni za kutosha. Vile vile, Bohari kuu ya Dawa (MSD) inaendelea na usambazaji wa dawa hizi katika vituo vyote nchini. Aidha, taratibu za kuagiza na kuleta shehena zaidi ya dawa za malaria kutoka nje ya nchi zinaendelea ili kuhakikisha kuwa dawa za kutibu malaria zinapatikana kwa muda wote.

 Regina L. Kikuli
KAIMU KATIBU MKUU
01/02/2013


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo