Prof. Maghembe
Mh. John Mnyika
NA RICHARD MAKORE
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemuweka katika wakati mgumu
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, baada ya kutoa hadharani namba
ya simu ya waziri huyo ili wananchi wamuulize ni lini atatekeleza ahadi
ya kuwapatia huduma ya maji wananchi wa jimbo hilo.
Mnyika alitoa namba ya simu ya Profesa Maghembe na Naibu wake, Dk.
Binillith Mahenge, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja
vya Goba mwisho na kuwataka wananchi kuwauliza viongozi hao wakuu wa
Wizara ya Maji ni lini watapatiwa huduma ya maji ambayo imekosekana kwa
zaidi ya miaka miwili sasa.
Mnyika alisema Profesa Maghembe akihututubia wananchi hao aliwapa namba
ya simu ‘feki’ na kwamba alifanya hivyo kutokana na kuwadharau.
Februari 17 mwaka huu, Profesa Maghembe akihutubia mkutano wa hadhara
eneo la Goba mwisho alikaririwa akisema kwamba huduma ya maji ingeanza
kupatikana Februari 20, mwaka huu, lakini hadi kufikia juzi ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Profesa Maghembe alikaririwa akisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) ndiyo ina funguo za kufungua maji ama kuyafunga na kuwataka
wananchi wa Kata ya Goba kumuamini kwamba Februari 20, mwaka huu
wangepata maji.
Mnyika alisema ni aibu kwa Waziri akiwa na viongozi wa kitaifa wa CCM
kutoa ahadi hewa na kwamba ataongoza maandamano makubwa ya wananchi wa
jimbo lake kuvamia ofisi za Profesa Maghembe kwenda kudai maji.