Askofu mkuu Dkt Alex Malasusa
Mzee wa Baraza la Wazee wa Mtaa wa
Kanani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Kaskazini Kati Arusha, Usharika wa Ngaramtoni, Daudi Loinyeye (56)
amefungwa kifungo cha nje cha miezi sita.
Amefungwa kwa kosa la kutishia kumuua kwa maneno Mwinjilisti wa usharika huo, Christopher Daniel (36).
Mwinjilishi Daniel alimfungulia Loinyeye mashitaka Julai 12 mwaka jana katika Mahakama ya Mwanzo ya Emaoi iliyoko wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha.
Juni 30 mwaka jana, mzee huyo wa kanisa alikamatwa wakati akiwa katika kikao cha hesabu za harambee.
Akisoma hukumu Ijumaa iliyopita katika mahakama hiyo, Hakimu Denis Shayo, alisema mahakama imebaini kuwa mshitakiwa alikuwa na chuki kubwa na mlalamikaji (Daniel) kwa madai ya kutumia vibaya fedha za harambee zaidi ya Sh milioni 20, zilizochangwa Machi 11 mwaka jana na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.
“Chuki hiyo imetokana na ubadhirifu wa fedha za harambee zaidi ya shilingi milioni 24 ambazo zilipatikana wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa la usharika huo,” alisema Hakimu
Alisema mahakama imesikiliza ushahidi wa pande zote na imeridhika na ushahidi wa mazingira na kuona kuwa kulikuwa na chuki kati ya mshitakiwa na mlalamikaji, hivyo imemtia hatiani mshitakiwa kuwa alitenda kosa hilo.
Hakimu Shayo alisema pamoja na shahidi wa pili wa mlalamikaji, Elphans Mereji (46) kukana kutofahamu njama za kupanga kumuua mwinjilisti Daniel, lakini alikana hivyo baada ya kubaini kuwa njama hizo zilijulikana.
Alisema shahidi wa kwanza wa upande wa mlalamikaji Christopher Ngungati (54) aliieleza mahakama kwamba Mereji alikwenda nyumbani kwake na kumweleza kwamba kipo kikundi cha watu, wakiongozwa na Loinyeye kimeandaa majambazi kwa lengo la kutaka kumuua Mwinjilisti Daniel na ameahidiwa kupewa Sh 300,000 kwa kazi hiyo.
Hakimu Shayo alisema mashahidi wa upande wa mshitakiwa, Emilina Stephen (36), Loning’o Loshinongi (45) na Dora Seuri (3), wote waliieleza mahakama kuwa kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo ilikuwa ya chuki.
Kwa mujibu wa Hakimu, mashahidi hao walisema kwamba mshitakiwa alifunguliwa kesi hiyo na mwinjilisti kwa lengo la kupunguza makali ya mzee huyo wa baraza, kuacha kumfuata na kutakiwa kutoa hesabu za harambee ya sh milioni 24.
Hakimu alisema pamoja na kusema hivyo mahakamani hapo, mashahidi hao walishindwa kutoa ushahidi wao kama mwinjilisti huyo anadaiwa fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, mahakama iliridhika na kuona kwamba kulikuwa na ushahidi wa mazingira na kuamua kumtia hatiani mshitakiwa kwa kifungo cha nje cha miezi sita na ndani ya kifungo hicho mtuhumiwa ametakiwa kutotenda kosa lolote.
Hata hivyo, Loinyeye amepinga hukumu hiyo na kusema sababu zilizotolewa na hakimu kwamba mashahidi wake hawakutoa vielelezo vya ushahidi wa ubadhirifu dhidi ya mwinjilisti haina msingi.
Loinyeye alisema kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo ni ya kutishia kuua kwa maneno dhidi yake na siyo ubadhirifu wa fedha za harambee na mashahidi walitoa ushahidi ni kwani nini kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama hiyo na wengine kukana kupanga njama hizo.
''Ninakata rufaa katika Mahakama ya Wilaya kupinga hukumu hiyo kwani haki yangu imechakachuliwa,'' alisema Loinyeye .
Mgogoro wa KKKT Usharika wa Ngaramtoni, Jimbo la Arusha Magharibi huo uliotokana na ubadhirifu wa fedha, uliwahi kuripotiwa na gazeti hili, ambapo Mkuu wa Jimbo, Mchungaji Godwini Lekashu alituhumiwa kutumia vibaya fedha hizo za harambee.
Hata hivyo, Lekashu aliripotiwa kukana shutuma hizo na kusema yeye siyo mmoja wa watuhumiwa. Mkuu wa KKKT, Askofu Dk Alex Malasusa aliunda Kamati ya maaskofu sita kutoka nje ya Dayosisi ya Kaskazini Kati Arusha, kuchunguza chanzo cha migogoro ili kupata undani wa tatizo na hatimaye kufikia hatua ya kuumaliza.
Hata hivyo migogoro ndani ya Dayosisi hiyo iliibuka mara baada ya Mchungaji Kiongozi, Philemon Mollel wa Usharika wa Ngateu, Jimbo la Arusha Magharibi kufukuzwa kazi na kusimamishwa kufanya shughuli za kichungaji katika kanisa hilo, kwa madai yasiyovumilika ndani ya kanisa.
Baada ya uongozi wa Dayosisi kuchukua hatua hiyo, washarika wa usharika wa Ngateu walipinga madai hayo, wakidai mchungaji huyo alichukuliwa hatua hiyo, kutokana na ukweli juu ya ubadhilifu uliofanywa na baadhi ya viongozi wa Dayosisi katika Hoteli ya Corridor Springs.
NA ZERO99BLOG