Si rahisi kuaminika, lakini
imetokea wilayani Kibaha mkoani Pwani, ambako mwanafunzi wa kidato cha
kwanza wa sekondari ya Pangani, akiwa na umri wa miaka 16 (jina
linahifadhiwa), ametekwa nyara na vijana watatu na kufungiwa ndani kwa
miezi minne.
Binti huyo, ambaye pia vijana hao walimtoa mimba wakitumia majani ya chai, katika eneo alilofichwa alijengewa mfano wa kaburi na kumlaza humo, huku juu yake wakiweka godoro na kutumia kama kitanda chao.
Akisimulia mkasa huo kwa mwandishi nyumbani kwao mjini hapa jana baada ya kufanikiwa kuwatoroka watekaji wake, binti huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kidimu wilayani hapa, alidai kutekwa na vijana hao Novemba 11, mwaka jana, saa tisa alasiri wakati akienda kanisani.
“Siku hiyo, babu ninayeishi naye alinihimiza nitangulie kanisani jioni, kwa kuwa alikuwa na shughuli anamalizia. Niliondoka mwenyewe, Kanisa letu liko mbali kidogo na nyumbani, njiani nilikutana na vijana hao watatu,” alisimulia binti huyo.
Alidai kuwa vijana hao walimsimamisha na kumsalimia, huku mmoja wao ambaye ni mkubwa, akimtaka waongozane hadi anakoishi (si mbali na eneo hilo) ili akamkabidhi mzigo wa mama yake mdogo (binti) ambaye anajulikana kwa jina la Martha.
“Kweli niliwaamini, kwa kuwa vijana wale nilikuwa nawaona mara kwa mara kijijini, ingawa mmoja wao alikuwa akijaribu kunipa vijizawadi nilikuwa nakataa, lakini siku waliponiambia wana mzigo wa mama mdogo sikuwa na sababu ya kukataa,” alisema.
Baada ya kufika eneo wanaloishi vijana hao aliowataja kwa majina ya Isaka, Faida na Jovian, walimkamata mkono na kumsukumia ndani, huku Faida ambaye alionekana kuwa mkubwa kuliko wenzake, akimwambia kuwa hayo ndiyo yatakuwa makazi yake kuanzia siku hiyo akiwa kama mkewe.
Mwandishi alishuhudia eneo la makazi ya vijana hao ambao waliwekwa hapo kama walinzi; nyumba ya chumba kimoja pembeni ndani ikiwa imepangwa matofali mfano wa kaburi, na juu yake kikipangwa miti kama chaga na godoro ambalo vijana hao walikuwa wakilipanga juu na kulala huku binti huyo akiwa uvunguni.
“Waliponikamata walitoa visu na kunitishia kuwa nikipiga kelele wataniua, wakanisukuma ndani na kuniingiza kwenye ‘kaburi’ hilo na kunilazimisha kulala huku juu wakiweka godoro, hata mtu akiingia ndani ya chumba hicho hawezi kujua kama mimi nimo,” alisema.
Alisema aliishi hivyo kwa muda huo wote, huku akila mlo mmoja kwa siku, kwani vijana hao, walikuwa wakiondoka nyumbani hapo alfajiri na kurejea saa saba usiku na kupika.
“Wakati mwingine wakirudi, Faida huwatoa wenzake nje na kubaki na mimi ndani, na kunilazimisha kuvua nguo na kunifanyia mchezo mchafu na kisha ananirudisha kwenye uvungu humo na wenzake kuingia kulala,” alisimulia.
Aidha, binti huyo, alidai kuwa kutokana na kuingiliwa kimwili mara kwa mara na kijana huyo, alipata ujauzito kwani alihisi baada ya kutapika na kupoteza siku zake, vijana wale walipogundua walihaha kutafuta dawa ya kutolea mimba, walichemsha majani ya chai na kumlazimisha kunywa.
“Baada ya kunywa chai hiyo nilikaa kwa saa tano hivi, nikaanza kupata maumivu makali tumboni na baadaye damu ilitoka kwa mabonge, wale vijana hawakunisaidia, zaidi ya kunitoa nguo zenye damu na kuchukua ule uchafu niliotoa na kuufukia nje,” alidai.
Aliendelea kudai kwamba kipindi chote hicho hakuwa na namna ya kutoroka, kwa kuwa waliweka mlinzi hadi aliposikia vijana hao wakigombania masuala mengine na mwenye eneo hilo ambaye aliwaitia polisi baada ya kutoelewana.
“Polisi walikuja pale, lakini nilishindwa kupiga kelele, kwa kuwa walinifungia kwenye chumba kile na Isaka ambaye alinishikia kisu wakati wenzake wamekimbia, polisi waliishia kuulizia walipoona wenyewe hawapo wakaondoka,” alieleza binti huyo.
Alidai kuwa Jumamosi iliyopita, vijana hao waliondoka kwenye chumba hicho alfajiri na mmoja wao akasahau kufunga mlango, ndipo akapata upenyo na kukimbilia porini ambako alikutana na msamaria mwema aliyemsaidia.
Binti huyo alidai kuwa mtu huyo mchoma mkaa alimsaidia kupitia porini hadi nyumbani kwao ili asikutane na vijana hao ambapo pia alimpigia simu babu yake na kwa kusaidiana na wakazi wa kijiji hicho na serikali za mitaa waliwasaka vijana hao na kuwakamata.
Babu wa binti huyo, Daudi Zakayo, alisema mjukuu wake huyo alipotea Novemba 3 na walifanya juhudi zote za kumtafuta ikiwa ni pamoja na kuripoti Polisi lakini bila mafanikio.
“Binti huyu ninaishi naye lakini baba yake yuko Ruvu anafanya kazi huko, mama yake hayupo, nilipoona haonekani nilimtaarifu baba yake, Charles Daniel, ambaye alikuja na wote tukaanza kuzunguka mtaani kwa rafiki zake hadi Polisi bila mafanikio,” alisema.
Alisema kutokana na binti huyo kutoonekana kwa muda mrefu, baba wa mtoto huyo alikwenda kwa waganga ambapo mmojawao alidai kuwa binti huyo yuko maeneo hayo amefichwa kwenye mti na mganga huyo kufanya mambo yake lakini hakuonekana.
“Nawashukuru wakazi wa eneo hili na Serikali ya Mtaa kwani baada ya kusikia mjukuu wangu amerudi walishirikiana nami na kumkamata kwanza Isaka, ambaye alikana kuhusika, lakini baada ya kucharazwa bakora, alitaja wenzake walipo, tuliwakamata na kuwapeleka kituo cha Polisi Tumbi,” alisema na kuongeza kuwa siku anamwona mjukuu wake, alimsahau kutokana na alivyochafuka na nywele zilivyomtimka.
Akizumgumzia tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa, Juma Yusuph, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwataja vijana wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na utekaji huo kuwa ni Faida Kazigwa, Isaka Kazigwa na Jovian Oswald.
“Kwa sasa vijana hawa wako chini ya ulinzi wanahojiwa kuhusu tukio hilo na ikithibitika kuwa wana kesi ya kujibu watafikishwa mahakamani,” alisema.
Mwandishi alifika hadi shuleni kwa binti huyo ambapo mlezi wa kike wa wanafunzi shuleni hapo, Mwalimu Bahati Eliaza, alikiri kusikia kuwa binti huyo amekumbwa na mkasa huo na kusisitiza kuwa wanasubiri taarifa ya Polisi ili wajue hatua zaidi za kuchukua.
“Sheria zinasema wazi, mtoto asipofika shuleni kwa zaidi ya siku 90 lazima jina lake lipelekwe kwa Bodi ya Shule ambayo itamjadili, lakini Katibu Tawala wa Mkoa akiwasilisha taarifa za mtoto na sababu za kutofika kwake shuleni, ataendelea na masomo, vinginevyo jina lake hufutwa,” aliongeza Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Peter Mihayo.
ZERO99BLOG