WAPIGA KURA JIMBO LA IRINGA MJINI WAMSHANGAA MBUNGE WAO

 
Na Fransis Godwin
WAKATI  mbunge  wa  jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa (pichani )na viongozi wa chama  cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) leo  walijitolea  kufanya usafi katika eneo la  kitanzani mjini Iringa kama njia ya kuhamasisha usafi, wapiga  kura  wa  jimbo  hilo wameonyesha kutofautiana na uamuzi huo wa mbunge  kufanya usafi  huku baadhi yao  wakidai  kuwa  jimbo hilo limemsinda kuongoza na ndio  sababu ya uchafu  kuzagaa kila kona ya mji .

" Mbunge  wetu leo anajitolea  kufanya usafi siku zote  alikuwa  wapi hadi uchafu unazangaa kiasi hiki  mitaani .....tunamtaka Msigwa  kufanya kazi kama  wabunge  wengine na kuachana na  siasa  za kuunga unga na kutafuta umaarufu kwa watu "

Wakizungumza l;eo  kwa nyakati  tofauti wananchi  wa jimbo la Iringa mjini  walisema  kuwa mji  wa Iringa  umeendelea  kuzidiwa na uchafu na kuwa mbali ya mbunge  kujitolea  kufanya usafi  pamoja na  wanachama  wa Chadema ila bado hatua hiyo haiwezi   kutatua tatizo la uchafu na badala yake uchafu  wa Manispaa ya Iringa  utaendelea kuwepo .

Juma  Husein mkazi  wa Kitanzini katika Manispaa ya Iringa  alisema kuwa mbunge  wao anatafuta umaarufu wa kisiasa na kusahau kuwa  yeye ni mbunge  wa  jimbo la Iringa mjini na mwakilishi  wa wananchi hao  bungeni  hivyo alipaswa  kutafuta  ufumbuzi  wa kudumu wa uchafu katika jimbo lake badala ya  kufanya usafi kwa misingi ya   kisiasa  huku akitambua  kufanya hivyo ni kujichongea  mwenyewe kwa  wananchi kuwa kumbe ameonyesha  kushindwa  kuongoza  jimbo hilo na ndio  sababu ya taka kuzagaa kila  kona.

Husein  alisema ni vema mbunge  Msigwa  kwenda  kujifunza katika  jimbo la Moshi mjini ambalo  pia linaongozwa na mbunge wa Chadema na kuona kama mbunge  huyo ametumia mbinu kama hiyo  kusafisha mji ama kuna mbinu nyingine  inatumika badala ya hiyo ya  zima moto  inayotumiwa na mbunge Msigwa  sasa ya  kukodi magari ya  usafi.

Aidha  alisema  kuwa kwa kuwa Manispaa ya Iringa  inakabiliwa na tatizo la magari ya  kusomba takataka na uhaba wa vyombo  vya kuhifadhia  takataka mbunge Msigwa  kwa  kutumia mfuko wa jimbo alipaswa  kuanza  kushughulikia kero  hiyo badala ya kukodi magari kwa  siku moja ili kutaka  kuonekana kuwa ni mchapakazi  wakati  siku  zote  yupo mjini Iringa na uchafu  huo  upo.

Kwa  upande  wake  mbunge Msigwa alipoulizwa na mwandishi wa  habari  hizi  kuhusiana na  utaratibu  huo  alisema  kuwa  kazi ya mfuko wa   jimbo  si kwa  ajili ya  kusafisha mji na kuwa yeye ataendelea  kusafisha mji kwa muda wa  siku  mbili  hizi kabla ya kwenda bungeni .

Msigwa  alisema  kuwa kupitia ofisi  yake tayari amekwisha  changisha  kiasi  cha shilingi  milioni  16 kwa  ajili ya kununua gari ya  kubeba taka katika Manispaa ya Iringa ili  kupunguza  tatizo la uchafu katika mji  huo.

Afisa  afya  wa Manispaa ya  Iringa  Severin Tarimo  alipotafutwa na  mwandishi  wa habari  hizi  ili kueleza  mikakati ya Manispaa ya Iringa  juu ya hali ya  uchafu  inayoendelea  kuukumba mji  huo  alidai kuwa kwa  sasa  yupo  likizo hivyo anayeweza  kujibia hilo ni yule aliyemwachia ofisi.

"Nazungumza na nani ....sasa  mimi  nipo  likizo bwana naomba uongee na mtu mwingine" alikata  simu


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo