Askari wa kike na wakiume wakimdhibiti kwa
bakora na marungu mwanafunzi wa chuo cha IFM (mwenye nguo za blue) baada
ya kumchomoa kwenye jengo alilojificha ili kukwepa mabomu ya machozi.
Huyu alishikiliwa mapema mara baada ya
mabomu kuanza kupigwa, huku akionja joto ya jiwe ya askari hao ambao
walionekana kuwa na uchu wakupiga.
SIKU moja baada ya
wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kuitisha maandamano
kushinikiza ulinzi wa polisi kutokana na vitendo vya udhalilishaji, jana
walielezea jinsi wanavyofanyiwa vitendo hivyo na wahuni.
Wanafunzi hao ambao wamepanga katika
nyumba zilizoko Kigamboni, wamedai kudhalilishwa na wahuni hao kwa
kuporwa vifaa vyao kama kompyuta, fedha na vitu vingine na hata kubakwa
na kulawitiwa.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi IFM
(IFMSO), Michael Charles jana alieleza jinsi udhalilishaji dhidi ya
wanachuo wawili wanaume wa chuoni hapo ulivyotokea Januari 12, mwaka
huu.
“Kulikuwa na wanafunzi wanne walikuwa wakijisomea chumbani kabla ya
kuvamiwa usiku wa manane na watu wasiowatambua wapatao wanane.”
“Watu hao walikuwa wanataka kompyuta,
simu, fedha na vitu vingine na vile ambavyo hawakuwa navyo, walizua
tafrani kati yao... Hawa jamaa walikuwa kwenye nyumba yao iliyoko Uwanja
wa Machava.”
“Katika sakata hilo, wanafunzi wawili
walipata upenyo na kukimbia, lakini wawili walikosa na kuendelea
kupambana na wahuni hao ambao waliwazidi nguvu kutokana na wingi wao na
kuwaingilia kinyume na maumbile.”
“Kwa kweli ilituuma sana baada ya
kupata bahari zile. Waliwadhalilisha sana... Jamaa walipora mali za
wanafunzi hao na zaidi ni kompyuta, fedha na simu. Tumekuwa tukiripoti
matukio haya mara kwa mara polisi, lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa kwani vitendo hivi ni vya muda mrefu.”
“Kuna siku nyingine, wanafunzi
walikuwa wakijisomea usiku, mara wakavamiwa na wahuni hao na
walipotakiwa watoe kompyuta, simu na fedha na pale inapotokea hawakuwa
navyo ama kuwabishia, basi wanajeruhiwa kwa mapanga.”
“Hiyo ni kweli kabisa, dada zetu
wanabakwa sana tu ila hawasemi kwa kuogopa aibu katika jamii na hata
taarifa zinapofikishwa polisi tunaishia kupewa RB tu halafu tunaambiwa
watafuatilia.”
“Hawa watu si kwamba ni wageni,
wanafahamika na hata maeneo yao wanayofanyia uharamia huo
yanafahamika... Ukweli wanatunyima uhuru kabisa na tumesharipoti polisi
lakini hakuna kinachoendelea. Tumeporwa zaidi ya kompyuta ndogo 300,
kinachotuuma zaidi, hawa wezi wanafahamika wanapokaa na polisi
inawaangalia.”
Wanafunzi wengine
Baadhi ya wanafunzi hao wanaoishi
Kigamboni walidai kuwa wanaishi katika mazingira hatarishi kwani wakati
mwingine uporaji hufanyika kweupe saa 11 jioni.
Maeneo yaliyotajwa kuwa ni hatari na
wakazi wa Kigamboni ambayo wenyeji hulazimika kuyapita kabla ya saa
12:00 jioni ni Midizini, Minazi Mikinda, Mnara wa Rada, Kisimani na
Serengeti.
Mwanachuo mwingine ambaye aliomba
jina lake lihifadhiwe alisema: “Tofauti za kimaisha baina yetu ndiyo
zinazosababisha chuki kuwa wanachuo wanaringa na kujiona wenye hadhi za
juu ndiyo maana wanafanyiwa vitendo hivyo.
Wakazi nao wanena
Baadhi ya wakazi wa
Kigamboni walisema kuwa mji huo ambao umepangwa kuwa wa kitalii sasa si
salama.
Mmoja wa wakazi hao ambaye pia
aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema inapofika saa moja usiku,
vitendo hivyo vya uporaji wa kutumia mapanga huanza na kuongeza kwamba
kinachowasikitisha ni Jeshi la Polisi kufumbia macho vitendo
hivyo.
Mwingine alisema wamekuwa wakipata usingizi wa shaka kutokana na
kujawa hofu kuwa muda wowote wanaweza kuvamiwa na kuporwa.HABARI ZAIDI BONYEZA HAPA>>>