UKEKETAJI MANYARA WAPIGWA MARUFUKU

 
MKUU wa Wilaya ya Hanang’  Mkoa wa Manyara Christina Mndeme amepiga marufuku mila potofu inayoendelea wilayani  hapo  ya kuwakeketa wasichana na atawachukulia hatua kali za kisheria wanaofanya kitendo hicho 
 
Taarifa hiyo ameitoa wakati akiongea na  waandishi wa habari  wilayani hapo mkoani Manyara.
 
Alisema kuwa  tabia ya baadhi ya watu wa jamii ya wabarbaig na wairaq kuendelea kuwakeketa watoto wao wa kike kwa njia ya siri inatakiwa kukomeshwa mara moja kabla hajachukua hatua.
 
 Pia alibainisha  kuwa japokuwa tabia hiyo imepungua kwa kiasi fulani wilayani humo lakini bado inaendelea kwa baadhi yao kuwafanyia mila hiyo potofu kwa kuwakeketa watoto wao wa kike kwa njia ya siri. 
 
 Aliendelea kusema kuwa madhara ya kuwakeketa wasichana ni makubwa kwani wanapata maumivu makali wakati wa kufanyiwa vitendo hivyo vya kikatili na pia wanaweza kuambukizwa maradhi pindi wakikeketwa.
Amewataka wakazi hao wabadilike kwa kuachana na mila potofu zilizopitwa na wakati kwani hivi sasa watu wengi wameshatambua kuwa kitendo hicho ni jambo la kikatili hivyo halipaswi kufanyika kama miaka iliyopita
 
 “Pamoja na matatizo hayo pia wakati wa kujifungua mama mjamzito anapata shida sana kutokana na kufanyiwa kitendo hicho hivyo jamii iache tabia hiyo mara moja kwani mila hiyo ni potofu na imepitwa na wakati,” alisema Mndeme.
 
 Nao baadhi ya wakazi  wa wilaya hiyo  wameeleza  kuwa hivi sasa vitendo vya ukeketaji vinafanyika kwa njia ya siri,baada ya jamii ya wairaq na wabarbaig ambao ni wengi wilaya humo kubaini kwamba Serikali haipendi jambo hilo kufanyika.
 
 “Watu wanaogopa Serikali na wanafanya vitendo hivyo kwa njia ya siri,kwa kuogopa kuwekwa ndani ila baadhi yao wanawakeketa wakiwa wadogo wengine wanagusa tu hilo eneo na wengine wanawapaka ugoro,” walisisitiza. 
 
  Walimalizia kwa kusema kuwa  baadhi ya watu wa vijiji vya Masqaroda,Gunyoda,Simbay,Getamuhog Gissambalang,Gidahababieg na Endasaboghechan vya wilayani hiyo,hadi hivi sasa bado wanaendelea na vitendo hivyo vya kukeketa wasichana.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo