PROF. MUHONGO ASHUKA MZIMA MZIMA NA KUTOA UFAFANUZI KUHUSU MIRADI YA UTAFUTAJI NA UVUNAJI WA GESI ASILIA NCHINI



DAR ES SALAAM, Tanzania
 
Kufuatia kuzuka maandamano na mijadala kuhusu miradi ya utafutaji na uvunaji wa gesi nchini, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Mhongo (pichani) ameshuka mzima mzima na kutoa taarifa ndefu kwa umma kufafanua mambo mbalimbali kuhusiana na sakata hilo. Mdau, Taarifa hii tumeitoa kama tulivyoipata na ni hii ifuatayo:

1.0 UTANGULIZI
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi  Asilia ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa yatakayopatikana kwa wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi. 

Siku ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara, wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya maandamano ya kudai raslimali ya Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania wote kwa kupitia vyombo vya habari.

Tokea Uhuru, uchumi wa Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile katani (Tanga na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa (Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na Mara),  chai (Iringa) na tumbaku (Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya nchi yetu  bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka mikoa hiyo hawajawahi kufanya maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania wengine) wa aina yo yote ile.  

1 Mapato  yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Tabora), almasi (Shinyanga) na tanzanite (Manyara) yamewanufaisha Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule! Minofu ya samaki wa Ziwa Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia Taifa letu fedha nyingi ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wo wote. 

Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote. Mahindi kutoka Rukwa, Mbeya, Ruvuma na Iringa yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu bila kujali eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi hayo ni kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na Kagera inatumiwa na wakazi wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya mikoa inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam bila manung’uniko yo yote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo cha Mto Ruvu. 

Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya wenyeji wa sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa. 

Kwa hiyo, kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo yote ile kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya Upinzani kupanga, kuhamasisha, kushabikia na kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara Mjini.
 
KUSOMA ZAIDI BONYEZA HAPA


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo