TAIFA letu limekuwa lilikabiliwa na
mdororo mkubwa wa uchumi uliosababishwa na sera ambazo si rafiki kwa
walalahoi. Suala la kuanzisha vijiji vya ujamaa kuliwaondolea motisha
wakulima na kuona kama kuna ukiritimba kwani aliyekuwa akifanya kazi kwa
bidii aliwekewa vikwazo.
Katika mkutano wa Taasisi ya
utafifiti katika masuala ya kiuchumi na kupunguza umasikini (REPOA)
uliofanyika Machi 28, mwaka huu Jijini Dar es Salaam, Profesa Ibrahim
Lipumba aliainisha baadhi ya masuala muhimu ya uchumi huku akiishauri
Serikali hatua za kuchukua.
Profesa Lipumba, ambaye ni bingwa wa
uchumi duniani, anasema wakati wa ujamaa wafanyabiashara wengi waliokuwa
katika sekta binafsi walikuwa wanajua namna ya kuitumia serikali na
sekta ya umma kuweza kupata masilahi ambapo kutokana na hali hiyo ndipo
rushwa ikaanza kwenye ukiritimba wa dola ndani ya uchumi.
Anasema, hadi kufikia mwaka 1985
Tanzania ilikuwa na hali mbaya zaidi kutokana na madeni yaliyoshindwa
kulipwa na Serikali hata kufikia Mashirika ya umma kupata hasara na
hayakuweza kuendeleza ajira wala uzalishaji.
Anasema, wakati tukiingia katika
urekebishaji wa uchumi huku tukiwa hatuna dira thabiti kwa wale
wanaouziwa mashirika, tulishindwa kujua waliouziwa kama wanaweza kufanya
kazi kama mikataba inavyosema.
Akitolea mfano, Profesa Lipumba
anasema, wakati wakulima wa korosho wanaambiwa wasimuuzie yeyote zao
hilo zaidi ya chama cha ushirika, bado chama hicho kinawakopa na
kusababisha kupungua kwa motisha kwa mkulima.
“Miundombinu yetu ni mibovu kwani
huwezi kuwa na uchumi wa kisasa bila ya kuwa na umeme wa uhakika,
uwekezaji wetu katika umeme umekuwa mdogo”
“Ni wazi uwekezaji mwingi ulikuwa
ukitegemea misaada kutoka nje, lakini pamoja na misaada hiyo, bado
tumeshindwa kukusanya mapato na kuendeleza uwekezaji nchini” anasema
Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi, anasema
anasema madini yamekuwa ni sababu kubwa kwa serikali kutegemea misaada
ya wahisani katika kupanga bajeti yake, kwani imekuwa haikusanyi mapato
katika sekta ya madini.
“Wawekezaji wamefanikiwa kututeka
kwani kampuni zote kubwa za wanasheria wetu maarufu ndio wanakuwa
wanasheria wa Kampuni za migodi, na Watanzania wengi maarufu wamepewa
nafasi ya kuwa wenyeviti wa bodi au wajumbe wa bodi.
“Kampuni zimekuwa bingwa wa kuchukua
watu wakubwa kuwa na vyeo vya juu, hivyo inahitaji kiongozi wa nchi uwe
na nguvu ya umma au jasiri kuhakikisha nchi nayo inapata fedha za
kutosha.
“Tanzania tumegundua kuwepo kwa gesi
maeneo ya Mkuranga, Mtwara na Kilwa lakini tusipokuwa makini kwa
kuangalia mikataba bado haitawanufaisha Watanzania.
“Tunatakiwa katika madini tupate
angalau mapato ya asilimia 30 yaingie katika pato la serikali ili
tuyaingize yasaidie katika sekta za afya, miundombinu, elimu na kilimo,”
anasema Profesa Lipumba
Anasema tofauti na hilo, inabidi
kujifunza kwa wengine huku akitolea mfano Botswana kwa kueleza kwamba
katika madini yao ambayo mengi ni almasi inayofikia asilimia 70,
inatumiwa kwa kuwanufaisha wananchi moja kwa moja au kuingia katika
mapato ya serikali au mapato ya umma.
Profesa Lipumba anasema nchi inapaswa kuwa na mikataba ya aina hiyo ambayo ina tija kwa wananchi.