Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro akisoma taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne katika Ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo
Wajumbe wakifuatilia kwa makini taarifa hiyo ya mkuu wa wilaya
Wilaya ya Makete hii leo imetoa taarifa ya mafanikio ya
serikali ya awamu ya nne tangu mwaka 2005-2012 kwa kuelezea mafanikio hayo
katika sekta mbalimbali kufuatia agizo la waziri mkuu Mizengo Pinda alilolitoa
kwa wakuu wa mikoa na wilaya kufanya hivyo
Akisoma mafanikio hayo mbele ya viongozi wa serikali na
binafsi pamoja na wananchi, Mkuu wa wilaya ya Makete mh. Josephine Matiro
amesema kuwa wilaya imepiga hatua katika nyanja mbalimbali zikiwemo elimu,
kilimo, afya, maji, na maliasili
Akizungumzia sekta ya kilimo mh. Matiro amesema wilaya
imekuwa na ongezeko la mavuno kutoka tani 74,219 mwaka 2005 hadi 145,436 mwaka
2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 95 huku matumizi ya pembejeo za kilimo
yakichangia ongezeko hilo
Amesema matumizi hayo ya pembejeo yanatumika katika shughuli
zote za kilimo ikiwemo mahindi na viazi
Pamoja na mambo mengine katika sekta hiyo pia serikali
imefanikiwa kujenga mifereji mitatu ya umwagiliaji kwani tangu mwaka 2005
mifereji hiyo haikuwepo ambayo ni mifereji ya Mfumbi, Luwumbu na Ikuwo na
miradi hiyo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 430
Kwa upande wa sekta ya afya mkuu huyo wa wilaya amesema
kumekuwa na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya hadi kufikia 41,
hospitali 3 vituo vya afya 5 na zahanati 33 huku vituo vya kutolea huduma za
unasihi na upimaji zikiongezeka kutoka vituo 3 mwaka 2005 hadi 15 mwaka 2012
Amesema idadi ya watu wanaopima virusi vya ukimwi kwa hiari
imeongezeka kutoka 109 sawa na asilimia 18 mwaka 2005 hadi 21,417 mwaka 2012
Akishukuru kwa niaba ya waalikwa waliofika kusikiliza
taarifa hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh. Daniel Okoka
ameshukuru kwa utaratibu huo ulioanzishwa na serikali huku akiikubali taarifa
hiyo na kusema ndiyo hali halisi
“sisi kama halmashauri
tunakubaliana na taarifa hiyo iliyosomwa na mkuu wa wilaya na imelenga karibu
sekta zote hivyo ni wajibu wetu kuzidi kufanya kazi ili taarifa ijayo ikija iwe
nzuri zaidi ya hapa” alisema Okoka
Amesema wilaya imepiga hatua ya kimaendeleo huku akitolea
mfano kuwa wilaya ya makete imejitahidi kujenga madaraja ya zege kwenye mito mikubwa iliyopo
wilayani humo tofauti na wilaya nyingine jambo linalopelekea TANROADS
kuipongeza wilaya kwenye vikao mbalimbali
“Ukiangalia kwenye mito
mikubwa yote tumejenga madaraja ya zege kwani ni ukweli usiopingika kuwa kuna
wilaya zinatumia madaraja ya miti hadi sasa, kwa kweli hili ni jambo la
kujivunia tena sana” alisema Okoka
Pia kwenye kikao hicho mkuu wa wilaya alitoa fursa ya wadau
mbalimbali walioshiriki kuchangia maoni ama kuuliza maswali kuhusiana na
mafanikio hayo, huku wadau hao wakitoa maoni yao pamoja na ushauri huku wengine wakiuliza
maswali ambayo yalipatiwa majibu kutoka kwa wataalamu waliohudhuria kikao hicho
Kutokana na agizo hilo
la waziri mkuu taarifa ya mafanikio ya serikali ya awamu ya nne itakuwa
ikisomwa kwa wananchi kila baada ya miezi minne