Na John J.Mnyika
Mwaka 2007 miaka miwili baada ya uchaguzi wa mwaka 2005
palijitokeza mjadala kuhusu sera ya majimbo. Mwaka 2012 ikiwa ni miaka
miwili
tena toka uchaguzi wa mwaka 2010 pameibuka kwa mara nyingine mjadala
kuhusu
sera ya majimbo kufuatia maandamano ya wananchi wa Mtwara juu ya madai
ya gesi.
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo amenukuliwa na gazeti
moja
tarehe 29 Disemba 2012 akiponda sera ya majimbo ya Chama Cha Demokrasia
na
Maendeleo (CHADEMA) kuwa ni mbovu na haitumiki kokote duniani; kauli
ambayo
haina ukweli kama nitavyoeleza katika makala hii. Amedai madai ya
rasilimali za wananchi wa eneo
hayana msingi na kuwaita wote wenye kujenga hoja hiyo kuwa wanataka
kuigawa nchi
vipande vipande, majibu ambayo ni mwendelezo wa propaganda chafu.
Prof. Muhongo badala ya kujibu hoja za waandamanaji na
wananchi wa Mtwara ameamua kuibua ‘vioja’ vya kuishambulia CHADEMA na
sera yake
ya majimbo. Wakati hata kwa sera za CCM na serikali ya sasa,
maandamano ya wananchi wa Mtwara kutaka majibu toka kuhusu manufaa ya
miradi ya gesi asili inayotoka katika maeneo yao ni matokeo
ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi na udhaifu wa Serikali katika
kuushirikisha umma katika michakato ya maamuzi ya kisera na kitaasisi
kuhusu rasilimali na
miradi muhimu ya maendeleo. Aidha, ni matokeo pia Bunge kutokuisimamia
kikamilifu Serikali kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa ibara ya 63 ya
katiba
wakati serikali inapoacha kufafanua masuala yanayohojiwa na wabunge na
inapokwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo
sekta
ndogo ya gesi asili.
Nashauri Rais Jakaya Kikwete apuuze majibu ya
Prof. Muhongo na atumie hotuba yake kwa
taifa ya mwishoni mwezi huu wa Disemba 2012 kueleza kwa umma undani wa
miradi
husika ya gesi asili na manufaa yake kwa
wananchi wa maeneo tajwa na nchi kwa ujumla; hatua ambayo alipaswa
kuifanya tarehe
8 Novemba 2012 wakati wa uzinduzi wa mradi
husika.
Nikirudi kwenye madai potofu ya Prof. Muhongo kuwa sera
ya majimbo ni mbovu, haitumiki kokote duniani na itaigawa nchi vipande
vipande,
nirejee majibu yangu ya mwaka 2007 kwa wasome na wanasiasa wenye mtizamo
kama
wake. Nikumbushe tu kwamba madai potofu kama hayo yalishika kasi sana
wakati wa
uchaguzi mkuu 2005 kwa vijembe vya majukwaani. Hoja kuu ya kufahamu ni
kwamba
chimbuko la sera ya majimbo nchini ni falsafa ya CHADEMA ya nguvu ya
umma.
Kwani umma ndio unapaswa kuwa na mamlaka lakini pia umma ndio unapaswa
kunufaika na rasilimali za nchi. Falsafa hii imeelezwa vizuri katika
ibara ya 3
ya katiba ya CHADEMA ambayo nashauri Prof. Muhongo na wote wenye mtizamo
kama
wake waisome na kuielewa.
