MWENYEKITI wa Halmashauri wa Wilaya ya Moshi
Vijijini, Morris Makoyi juzi alilazimika kuongoza mamia ya waombolezaji kutimua
mbio kuokoa roho zao, baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki msibani.
Tukio hilo la aina yake na lisilo la kawaida, limetokea
baada ya kuzikwa marehemu Agnes Malya aliyekuwa na umri wa miaka 30, ambaye
inadaiwa ameacha wosia kuwa kusiwe na mbwembwe kama vile vyakula, pombe, suti
na sare nyingine wakati wa mazishi yake.
Katika mbio hizo, Makoyi aliongozana na Paroko wa Parokia ya Mkombole, aliyefahamika
kwa jina moja la Ephraim waliacha magari ya kifahari waliyofika nayo msibani na
kukimbilia migombani.
Nyuki hao, wakiwa katika makundi makubwa matano walijitokeza na kuanza kuwashambulia waombolezaji, baada ya mazishi ya marehemu Malya aliyezikwa katika Kijiji cha Osaki huku tukio hilo, likihusishwa na madai ya kupuuzwa kwa wosia wa marehemu ambaye alipinga kuandaliwa vyakula na vinywaji, vitu ambavyo vitagharimu fedha ambazo zingetosha kugharamia matibabu yake, kutokana na ugonjwa wa kansa ya ziwa uliogharimu maisha yake.