Na Nickson Alex
MKUU wa mkoa wa Njombe Captain mstaafu Aseri Msangi amenusurika kufa maji katika mwambao wa ziwa nyasa na kulazimika kukatisha ziara yeye na msafara wake kutokana na ziwa hilo kuchafuka ghafla kwa dharuba na mawimbi makali.
Msangi alikutana na sintofahamu hiyo baada ya kumaliza mkutano wa hadhara katika kijiji cha makonde na kulazimika kuacha boti alilokuwa akisafiria na kuamua kutembea kwa mguu kwa takribani masaa matatu kutoka makonde hadi kata ya Lifuma.
Kwa mujibu wa ratiba mkuu wa mkoa na msafara wake alianza ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika mwambao wa ziwa nyasa.
Ambapo ilikuwa afanye mkutano wa hadhara katika kata ya Lupingu siku hiyo ya jumatatu.
Mkuu wa mkoa alisafiri kwa boti la halmashauri hadi kata ya Makonde ambako alifanikiwa kufanya mkutano lakini kwa shida kutokana na wananchi wa kijiji cha makonde kujaribu bila mafanikio kuharibu mkutano huo kwa kuandika mabango ya kumtaka mkuu huyo kuondoka na diwani wao Cryspin mwendapole mwakasungura kwa tuhuma za ufisadi ambazo hata hivyo walishindwa kuzidhibitisha.
Baada ya mkutano huo uliojaa vijembe na kiburi cha kumtaka diwani aendolewe kienyeji kumalizika na msafara kutakiwa kuondoka kuelekea kata ya Lifuma ndipo ghafla ziwa likachafuka na kulazimika kutembea kwa mguu.
Aidha mkuu wa mkoa alilazimika kulala siku mbili katika kasiri ya kanisa katoliki kutokana na ziwa hilo kuendelea kutishia usalama wa msafara huo ambapo kila kukicha mawimbi yalikuwa yakiongezeka na kupelekea kushindwa kuendelea na ziara.
Akitoa ratiba ya ziara mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha alilisema kuwa mkutano wa hadhara ulitakiwa kufanyika kata ya Kilondo na kata ya Lumbila na kisha kuunganisha hadi Matema Kyela mkoani mbeya lakini ilishindikana kutokana na kuongezeka kwa dhoruba.
Hata hivo Madaha akaongeza kuwa ziara imesitishwa hadi desemba 12 mwaka huu ambapo sasa ziara itaanzia kyela na kuzifia kata ya Lumbila na Kilondo.
Mkuu wa mkoa pamoja na mambo mengine alipita kuzungumza na wananchi pia kuwaondoa hofu kufuatia mzozo na mvutano wa mipaka unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi.
Tarafa ya mwambao wa ziwa nyasa ina kata za Lupingu, Ilela, Lifuma, Kilondo na Lumbila ambazo wananchi wake wanategemea uvuvi duni wa samaki kuendeshe maisha yao ya kila siku.