MGAMBO MAKETE WATAKIWA KUTOSHIRIKI KWENYE VITENDO VYA KIHALIFU

 Mgambo wenyewe
 Mshauri wa mgambo wilaya ya Makete Bw. Mfuse
 Mgambo akisoma risala kwa mgeni rasmi


 Mkuu wa wilaya akigawa vitambulisho kwa mgambo
 Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro(wa pili kulia) akicheza muziki na mgambo hao

Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro

Imeelezwa kuwa mgambo wanatakiwa kuwa raia wema na ni chombo ambacho hakitakiwi kunyanyasa ama kubugudha raia kwani ni njia mojawapo itakayoongeza imani kwa jamii juu ya chombo hicho

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni kamanda wa mgambo wilaya Mh. Josephine Matiro wakati akifunga rasmi mafunzo ya mgambo wilaya ya Makete hii leo katika uwanja wa joshoni kata ya Iwawa wilayani hapo

Amesema inasikitisha kuona wanamgambo ambao wanatakiwa kulinda raia na mali zao pamoja na kudhibiti vitendo vya kihalifu katika maeneo yao nao wanakuwa wahalifu

“Unajua ninyi ni watu muhimu sana katika ulinzi wa maeneo yenu hivyo mnatakiwa muwe makini msijihusishe na vitendo vya kihalifu ili muwe mfano bora kwa jamii na jamii iwaamini” alisema Matiro

Amesema suala la mgambo lipo na linatambulika kisheria huku akiwasisitiza kutokatishwa tama na mtu yeyote kuwa kazi ya mgambo haifai na haina maslahi yeyote kwa jamii hivyo wasijihusishe nayo na badala yao waongeze juhudi ya kupambana na vitendo vya kihalifu katika maeneo yao

Katika hatua nyingine mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa kufungua kambi ya vijana kwa lengo la kuzidi kuwaweka pamoja huku pia akiwataka kuomba nafasi mbalimbali za kazi zenye sifa za mgambo pindi zinapotangazwa wilayani hapo kwa kuwa watapewa kipau mbele

Akisoma risala kwa niaba ya wenzao mbele ya mgeni rasmi mmoja wa mgambo hao Bw. Aldo Sanga amesema wamefurahia mafunzo hayo ingawa yalikuwa na changamoto za hapa na pale lakini wamefanikiwa kufuzu

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa vitendo vya rushwa vilivyotolewa na baadhi ya watu ili wasishiriki mafunzo hayo, rushwa na upendeleo wakati wa ajira mara baada ya kufuzu mafunzo pamoja na baadhi ya wanajamii wengi kuwadharau mgambo hao hasa wakati walipokuwa wakishiriki mafunzo hayo

Akitoa taarifa fupi mbele ya mgeni rasmi Mshauri wa mgambo wilaya, Afisa mteule daraja la pili Bw. Mfuse amesema katika kituo cha Iwawa walijiandikisha watu 137 lakini hadi wanahitimu hii leo walikuwa 85 wanawake 12 na wanaume 73

Amesema wakati wa mafunzo hayo ya miezi mine walifundishwa mbinu mbalimbali za kijeshi, masomo ya uraia na matumizi ya silaha na walishiriki shughuli za kijamii ikiwemo kuchimba choo cha kijiji pamoja na kushiriki kuzima moto kichaa

Hali kadhalika mkuu huyo alifunga mafunzo hayo kwenye kituo cha Tandala ambapo waliojiandikisha walikuwa 63 na hii leo wamehitimu 37 wakike 2 na wakiume 35


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo