Onyo limetolewa kwa wakazi wa Makete mjini eneo la sokoni ambao wanajisaidia maporini wakati huu ambao choo kipya cha soko la Makete mjini kinajengwa kutokana na walichokuwa wakikitumia awali kujaa, kuacha tabia hiyo mara moja kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi wakikamatwa
Onyo hilo limetolewa na Afisa Afya wilaya ya Makete Bw. Boniphace Sanga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo
Bw. Sanga amesema kwa mujibu wa sheria za afya ni kosa kwa mtu kujisaidia vichakani ama misituni kwa kuwa suala hilo linahatarisha afya za wengine kwani ni rahisi magonjwa ya milipuko kutokea
“Mimi nashangaa mpaka karne hii watu wanajisaidia maporini, yaani hata mtu anashindwa kwenda kujisaidia kwenye vyoo vya kwa majirani mpaka aende maporini huko, kwa kweli watu wa hivyo hata nyumbani kwao utakuta hivyo hivyo, hiyo ndio tabia yao ” alisema
Ametoa wito kwa wakazi wa maeneo yao ya sokoni kuwapiga picha wale wote wanaokwenda kujisaidia maporini halafu picha zao zibandikwe kwenye mbao za matangazo ili iwe fundisho kwa wengine, na wakati mwingine wawakamate na kuwapeleka kwenye ofisi yao ili hatua za kisheria zichukuliwe juu yao
“Wakazi hao wawapige picha halafu picha zao wazibandike kwenye mbao za matangazo tuone nani anayependa aibu, wataacha tu” alisema Sanga
Awali wakizungumza na wanahabari waliofika maeneo hayo kushuhudia ujenzi huo wa choo, wakazi hao wamesema baadhi ya watu wamekuwa wakienda kujisaidia kwenye mapori yaliyopo karibu na soko hilo hali ambayo inahatarisha usalama wakazi wa eneo hilo
“Mambo gain haya jamani, mtu mzima na akili zake halafu anakwenda kujisaidia pale(akipanyooshea kidole), hivi kweli hii ni akili au matope jamani tumechoka, vyoo vya majirani vipo lakini wao wanakwenda pale, inasikitisha sana na mvua hizi yaani sijui itakuwaje” alisema mkazi mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake
Hivi sasa soko la makete mjini linaendelea na ujenzi wa choo sokoni hapo kutokana na kilichokuwepo kujaa