Na Furahisha Nundu
Wananchi wa kijiji cha Ivalalila wilayani Makete wameaswa kutoanzisha moto ovyo katika mazingira yao ili kupunguza athari zitokanazo na madhara ya moto.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho Afisa mtendaji wa kijiji Bw.Fidelisi Sanga amesema kwamba moto umekuwa ukitoroka mara kwa mara na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za watu na mazingira kiujumla.
Ameongeza kuwa moto huo umekuwa ukisababishwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wachoma mkaa na waandaaji wa mashamba, na kwa kiasi kikubwa huchomwa miti inayosababisha upatikanaji wa mvua na inayotunza vyanzo vya maji.
Kwa upande wao Bw. Deo Chaula na Bw.Asheri Mbilinyi wamesema zaidi ya hekari nane za mashamba ya miti zimeteketezwa na moto
Hata hivyo wananchi hao wamedai kuwa faini zinatozwa kwa sasa shilingi elfu hamsini ni ndogo hivyo wameomba kuongezwa kwa adhabu hiyo mara mtuhumiwa anapopatikana na kosa la aina hiyo.