Wanafunzi wakiwa wamenyanyua juu mabango yenye ujumbe wa kutomtaka mkuu wa shule
Habari imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Pamela Mollel
MKUU wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo amewasweka lumande wanafunzi
watatu wa Shule ya Sekondari Kimnyaki kwa kosa la kushinikiza maandamano
ya wanafunzi wenzake hadi Ofisini kwake.
Wanafunzi hao waliokamatwa kwa kosa la kuchochochea maandamano hayo
ni pamoja na Ezekiel Memiri, Losijaki Lunde, na Meshack Lomunyaki.
Maandamano ya wanafunzi hao yalikuwa na lengo la kumshinikiza Mkuu huyo wa Mkoa kumuondoa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule hiyo jana Ofisini kwake alisema
kwamba wanafunzi hao wameshindwa kufuata maagizo yaliyoandikwa katika
fomu zao za kujiunga na masomo shuleni hapo.
Mkuu wa Mkoa alisema kwamba ni makosa makubwa kwa wanafunzi kukaidi
ama kushindwa kufuata maagizo ya shule hasa yaliyoandikwa katika fomu
zao za kujiunga na shule.
“Askari kamata hawa jamaa weka ndani hawana heshima hata
kidogo,haiwezekani wakalifanya jiji la Arusha kama kiwanja cha michezo
kwamba kila anayehitaji kucheza anaruhusiwa kufika, haya mambo
hayawezekani hata kidogo, lazima utaratibu ufuatwe na kila mmoja apewe
haki ya kusikilizwa” alisema Mkuu wa Mkoa na kuongeza: “Tena nataka
kuchukuwa nafasi hii kupiga marufuku maandamano yote ya wanafunzi katika
Jijini la Arusha, siwezi kukubaliana na suala hili hata kidogo, kuna
viongozi wa serikali wapo shuleni, nyinyi mko huku, Mkuu wa Wilaya ya
Arumeru yuko huko tayari kwa ajili ya kuwasiliza mmekimbilia kwa Mkuu wa
Mkoa tena bila vibali vya maandamano”
Awali kabla ya wanafunzi hao kufika Ofisini kwake walikutana na
vikwazo vya Askari wa Jeshi la Polisi na kuwapiga mabomu ya machozi
wanafunzi hao.
Maandamano hayo yaliyoanza juzi kwa lengo la kumshinikiza Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo aondolewe kwa kile walichodai kwamba anachangia
kudidimiza maendeleo yao kitaaluma na kwamba anafurahia matokeo mabaya
ya wanafunzi hao baada ya mitihani yao.
Baada ya Jeshi la Polisi kufanikiwa kuzuia maandamano hayo siku ya
kwanza, jana wanafunzi hao walibuni njia nyingine ya kuandamana na
kufanikiwa kufika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
“Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru alifikia shuleni kwetu akatuambia
kwamba angekuja kesho (Jumnne) tukamsubiri hadi saa nne bila mafanikio
ndipo tulipobuni njia nyingine ya kuandamana, tukaamua kuondoka shule
mmoja mmoja mpaka katikati ya mji, na tulipokutana na askari hao
tukaanza tena kupambana na kila walipoturushia mabomu ya machozi sisi
tuaanza kuwarushia mawe huku tukinawa usoni,” alisema Ezekiel Memiri.