Faraja Mlelwa, diwani mteule wa Mlangali CHADEMA
Wapiga kura wa kata ya Mlangali wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wamemgaragaza vibaya mgombea wa Chama cha mapinduzi (CCM) Bw.Andrew Mhagama aliyewahi kukitumikia chama hicho kama katibu wa chama kwa wilaya mbalimbali nchini na baadaye kustaafu na kumchagua mgombea wa Chadema Faraja Mlelwa.
Uchaguzi huo umefanyika baada ya aliyekuwa Diwani Bw.Kacheche kufariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba chumbani kwake kwa sababu zisizo fahamika mwanzoni mwa mwaka 2012.
Katika uchaguzi huo mgombea wa Chadema Bw Faraja ameshinda kwa tofauti ya kura 163 dhidi ya mgombea wa CCM Mzee Mhagama na hoja kubwa ya kufanya wapiga kura kutomchagua Mhagama ni kuwa ni mzee ambaye itakuwa vigumu kufanyakazi na mbunge wa jimbo hilo Deo Filikunjombe (CCM) ambaye ni kijana.
Awali katika kampeni za mwaka 2010 Bw.Filikunjombe ambaye ni mbunge wa jimbo la Ludewa alinukuliwa na wananchi hao akisema”nipeni mimi kura zote kwani ni kijana na kijana anaweza kufanyakazi zaidi ya mzee”,Mzee ambaye alikuwa ni mpinzani wake Prf.Mwalyosi.
Hivyo hata kampeni za kumsaidia Mhagama Bw.Filikunjombe alikutana na maswali mengi kutoka kwa wananchi wake ya kumuuliza kwanini aliwaletea mzee wakati katika kampeni zake alisisitiza wachaguliwe vijana ili walete mabadiliko ya kimaendeleo.
Bw.Filikunjombe alionekana kushikwa na kigugumizi na kuwataka wananchi kumchagua mzee huyo ili kuweka uwiano ndani ya chama cha mapinduzi kwani wazee ni washauri wakuu ndani ya chama chao.
“Kunichagua mimi kama kijana isiwe fimbo kwa wengine tutambue wazee ndio washauri wetu wakubwa hivyo kama madiwani wetu watakuwa vijana na wazee utendaji kazi utakuwa mkubwa kutokana na ushauri watakaoupata vijana kutoka kwa wzeee”,alisema Filikunjombe katika kampeni hizo.
Hata hivyo wananchi wa kata ya Mlangali walionekana kutoridhishwa na majibu ya mbunge wao na kubaki na msimamo wao wa kuchagua kijana ambaye ataendana kiutendaji kazi na Bw.Filikunjombe ambaye ni kijana.
Msimamizi wa uchaguzi wa kata hiyo Bw.Broun Kilanga alimtangaza mgombea wa CHADEMA kuwa mshindi na ndiye atakayekuwa Diwani mpya wa kata hiyo kwani alimsinda mpinzani wake kwa zaidi ya kura 163.
Bw.Mlelwa ameweza kuibuka mshindi kutokana na sababu za kuwa kijana mdogo mwenye elimu kubwa kwani ana shahada mbili hivyo kampeni zao na mwenendo wa uchaguzi mzima ulikuwa wa huru na haki pia amani ilitawala katika mikutano mbalimbali ya kampeni zao.