MKUTANO wa Tisa wa Bunge la Muungano
unatarajia kuanza kesho Mjini Dodoma, huku ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge
iliyoundwa kuchunguza tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge ikisubiriwa kwa
hamu kubwa.
Tume hiyo inayoongozwa na Hassan
Ngwilizi iliundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya kuchunguza
tuhuma hizo zilizoibuka katika mkutano wa Bunge uliopita. Tuhuma hizo ndizo
zilizomfanya Spika kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo,
Agosti mwaka huu, Makinda aliunda tume ya wabunge watano kuchunguza tuhuma
hizo.
Ripoti hiyo inatarajiwa kuwa mtihani
mkubwa kwa Spika Makinda hasa ikizingatiwa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya
kuwasilisha ripoti hiyo bungeni hasa kutokana na kuibuka kwa maneno ya
chinichini kwamba kumekuwa na jitihada za kuwasafisha wabunge hasa wa chama
tawala.
Hivi karibuni, Naibu Spika, Job
Ndugai alikaririwa akisema kuwa mamlaka ya namna ya kuiwasilisha ripoti hiyo
yako mikononi mwa Spika Makinda.
“Kwa kawaida na kanuni zetu ni
kwamba Spika anaweza kuamua kama ripoti hiyo ijadiliwe au iwasilishwe kwa njia
ipi, wala hawezi kuingiliwa,” alisema Ndugai.
Mbali na ripoti hiyo, Mkutano huo wa
Bunge ambao utadumu kwa wiki mbili, pia unatarajiwa kupokea hoja binafsi kutoka
kwa Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jaffo kuhusu mifuko ya jamii.
Jaffo aliibua hoja hiyo katika
mkutano uliopita akitaka itungwe sheria ya kufanya marekebisho ili kipengele
kinachomtaka mwanachama wa mfuko kupewa mafao yake pindi anapofikisha umri wa
miaka 55 kiondolewe.
Wakati huohuo, Wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi walianza kuwasili
Dodoma jana tayari kwa mkutano wa uchaguzi unaotarajia kuanza kesho.
Awali, mkutano huo uliokuwa ufanyike
Oktoba 27 hadi 28, lakini ulisogezwa mbele ili kupisha waumini wa dini ya
Kiislamu kuungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haj.
Katika uchaguzi huo nafasi ya
mwenyekiti inagombewa na Abdallah Bulembo na John Barongo na Martha Mlata.
Tayari Jumuiya nyingine za CCM za
Umoja wa Vijana (UVCCM) na UWT zimeshafanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa
kuziongoza kwa kipindi cha miaka mitano. (source:mwananchi)
|