Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier
Daudi amewataka wahitimu na wale wote wenye kutafuta fursa za ajira
Serikalini kujijengea utamaduni wa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya
Ajira mara kwa mara kwani kila nafasi za ajira zinapojitokeza huwekwa
katika tovuti hiyo ili kutoa fursa kwa wadau walioko nje na ndani ya
nchi kuweza kuziona kwa urahisi.
Daudi
amesema, kwa mfano mwananchi yeyote akitembelea katika tovuti ya
Sekretarieti ya Ajira hivi sasa ataona tangazo la kuitwa kazini kwa
waombaji kazi waliofaulu katika usaili uliofanyika mwezi Juni, 2012
ambao wanatakiwa kuripoti kwa Waajiri; Wakala wa Vipimo, pamoja na kwa
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mbali na hilo, pia
watakuta tangazo la kuitwa kwenye usaili kwa wale waliokidhi vigezo
kulingana na nafasi walizokuwa wameomba kama zilivyokuwa zimetangazwa
kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha Mipango Dodoma,
Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Chuo cha Serikali za Mitaa
Hombolo na taasisi nyinginezo.
Aliongeza kuwa katika Tovuti hiyo
watakuta pia tangazo la nafasi za kazi 194 zikiwemo nafasi za
Wakurugenzi, Wakufunzi Waandamizi wa Vyuo, Wakufunzi Wasaidizi,
Wahandisi, Mafundi Sanifu, Wakaguzi wa ndani wa hesabu, Makatibu
Mahsusi, Walinzi, Wapishi na kada nyinginezo.
Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti ya tangazo pindi wanapotuma maombi yao kwa njia ya posta ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata fursa ya ajira serikalini maana mchakato wa ajira hufuata Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira alimaliza mahojiano yake kwa kuitaja tovuti ya Sekretarieti ya Ajira kuwa ni www.ajira.go.tz kwa wale wasioifahamu ili waweze kuifahamu.
