Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa
Tabora, Mhe. Fatma Abubakar Mwasa kufuatia taarifa za vifo vya watu 17
wakiwemo watoto watano vilivyosababishwa na ajali ya Basi la Kampuni ya
Sabena iliyotokea katika eneo la Kitunda, Wilaya ya Sikonge Mkoani
Tabora siku ya Jumanne tarehe 7 Agosti,
2012.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na
taarifa za vifo vya watu 17 waliofariki papo hapo baada ya Basi la
Abiria la Kampuni ya Sabena kupata ajali katika eneo la Kitunda Wilayani
Sikonge katika Mkoa wa Tabora”, amesema Rais Kikwete katika Salamu
zake za Rambirambi na kuongeza,
“Kwa mara nyingine tena tunashuhudia kupotea kwa
maisha ya ndugu zetu 17 wasiokuwa na hatia kutokana na ajali za
barabarani za mara kwa mara ambazo busara na hekima ya madereva na
uwajibikaji wa pamoja wa vyombo vyenye dhamana na usimamizi wa Sheria ya
Usalama Barabarani vinahitajika sana kuepusha vifo vya aina hii”.
“Kwa dhati ya moyo wangu, ninakutumia wewe Mkuu
wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Fatma Mwasa Salamu zangu za Rambirambi na
pole nyingi kutokana na msiba huo mkubwa uliotokea Mkoani kwako. Aidha
naomba unifikishie rambirambi hizi kwa ndugu na jamaa wa watu wote
waliofikwa na msiba huu. Nawaomba wote wawe na moyo wa uvumilivu na
subira wakati huu wa kuomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao.
Ninawahakikishia kuwa niko pamoja nao katika maombolezo haya”,
ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es
Salaam.
9 Agosti, 2012