KONDA AKIWA KWENYE DALADALA
Tarime
Mamlaka ya udhibiti wa
usafiri wa majini na nchi kavu SUMATRA mkoani Mara, imewaagiza wamiliki wa
magari madogo ya abiria wilayani Tarime, kuzingatia nauli elekezi zilizopangwa
na mamlaka hiyo na kuonya kuwa wamiliki watakaobainika kuendelea kutoza nauli
ambazo ni kinyume na viwango hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo
kufungiwa leseni zao.
Agizo hilo limetolewa mjini
Tarime na Afisa mfawidhi wa Sumatra mkoa wa Mara, Kapteni Michael Rogers,wakati
wa zoezi la ukaguzi wa magari ya abiria yanayotoa huduma kati ya wilaya ya
Tarime na miji ya Musoma na Mugumu pamoja na maeneo ya Sirari, Nyamongo na
Shirati katika wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Kaimu kamanda wa kikosi cha
usalama barabarani Kanda Maalum ya Tarime/ Rorya, mkaguzi wa polisi Charles
Ntenga, amewashauri wananchi kutoa ushirikiano kwa askari wa usalama barabarani
kuhusu magari yanayoendelea kutoza nauli kubwa tofauti na viwango vya Sumatra,
huku akiwaonya wale watakaojaribu kuchezea sheria.
Katibu wa chama cha wamiliki
wa magari madogo ya abiria wilayani Tarime Kazimoto Kabila, pamoja na baadhi ya
wadau wa usafirishaji na abiria wamesema SUMATRA inapaswa kufikiria upya
viwango vya nauli kutokana na kupanda kwa bei za mafuta, vipuri vya magari na
kuharibika kwa miundombinu ya barabara ili waweze kuendesha biashara zao kwa
faida.