
Waandishi
wa habari wakimfuata Balozi Profesa Mahalu akiwa pamoja na Mdogo wake
Mirasi Rama wakitoka nje ya Mahakama ya Kisutu Mchana huu mara baada ya
kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili.
MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo imemuachia huru Bila hatia aliyekuwa
Balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala
wa ubalozi huo, Grace Martin waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu
Uchumi na Kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni.
Hukumu hiyo kwa Profesa Mahalu na Martin imetolewa na Hakimu
Mfawidhi mkazi wa Mahakama ya Kisutu Mh. Ilivin Mugeta kwa kumuachia
huhu mahalu ambaye alikuwa akitetewa na mawakili wakongwe Mabere
Marando na wenzake.
Prof. Mahalu alikuwa akikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya
uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60,
katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini
Italia.
Hukumu ya kesi hiyo iliyokuwa ikinguruma mahakamani hapo kwa
miaka kadhaa sasa, imefikia tamati leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ambaye amekuwa akiisikiliza.
Awali, hukumu hiyo ilipangwa kusomwa Julai 11, mwaka huu lakini
iliahirishwa kutokana na Hakimu Mugeta kukabiliwa na majukumu mengine.
Kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na kupanga
kuwa hukumu hiyo itasomwa leo.
Kiongozi wa jopo la mawakili
wa washtakiwa hao, Mabere Marando alisema jana kwamba anaamini kesi
hiyo ambayo imechukua muda mrefu, leo inafikia mwisho kwa Mahakama
kutoa hukumu.
Endapo Mahalu na Mwenzake katika makosa kama hayo yaliyokuwa
yakiwakabili wangepatikana na hatia adhabu yake ingeweza kuwa kifungo
kisichozidi miaka 15 jela.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi,
Kifungu kidogo cha pili, Mahakama inaweza kutoa amri nyingine ikiwamo
mshtakiwa kulipa fidia.
Hukumu ya kesi hiyo leo ilikuwa ikisubiriwa na kwa shauku si tu
na Profesa Mahalu na wenzake ambao wangependa kujua hatima yao, bali
pia na umma wote wa Watanzania ambao umekuwa ukiifuatilia kwa muda wote
kesi hiyo.
Wakati wa utetezi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye
ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake, alipanda
kizimbani na kumtetea Profesa Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato
wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata sheria.
Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa
mchakato huo ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia
alimmwagia sifa kedekede Profesa Mahalu akidai kuwa ni kiongozi
mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa umma.
Akiongozwa na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake,
Alex Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo
na malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
Wakati upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi
kutokana na kuwapo kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo,
Mkapa alidai kuwa aliifahamu mikataba yote hiyo na malipo kufanyika
kupitia akaunti mbili tofauti.
Alieleza kushangazwa kwake kusikia kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu
Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa
hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, akisema hajui ni kwa nini
Lumbanga alisema hivyo.
Mbali na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ambayo wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye
aliyekuwa waziri wake, Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni
Ujenzi na ile ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda
kufanya tathmini ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake.
Alisema taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo,
Kikwete bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo ni sahihi.
Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo
lilinunuliwa kwa Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake
zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
“Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo
ninayoyajua mimi,” alisema Mkapa na kuongeza kwamba hajawahi kupata
malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria wakati wa mchakato
wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki akidai kuwa alilipwa pungufu
ya makubaliano.
Akijibu swali la Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko
yoyote kutoka kwa CAG kuhusu ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa
hajawahi kupokea malalamiko hayo.
Akijibu swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama
aliwahi kuuliza ni kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia
mikataba miwili, Mkapa alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa
anahitaji ni kupata jengo.
Akijibu swali kwamba kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa
kwa mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake,
Mkapa alijibu: “Hilo ni tatizo lake na nchi
yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema
Alhamdulillah.”
Pia Mkapa alisema anamshangaa wakili wa Serikali kudai kuwa
pesa hizo kulipwa kwa awamu mbili kunaonyesha kwamba Profesa Mahalu
alikuwa na lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake... “Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa
nitakushangaa wewe maana Profesa (Mahalu) mimi namwamini.”
Utetezi wa Profesa Mahalu
Katika utetezi wake, Profesa Mahalu alikana mashtaka hayo na
kudai kuwa alipofika katika ubalozi huo alikuta ofisi hizo zikiwa na
hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake za mfukoni na kununua
samani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi.
Alisema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Kikwete pia alifika katika ofisi za ubalozi huo na
kushuhudia hali hiyo mbaya na kwamba aliunga mkono hoja yake kwamba
ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya
ubalozi.
Alisema mwanzoni mwa Juni, 2001 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya
kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge.
Alidai kuwa Katibu Mkuu alimtaka yeye na maofisa wengine wa
ubalozi kuanza kutafuta majengo. Alisema baada ya hapo aliwaagiza
maofisa wake kwenda kutafuta majengo ndani na nje ya Jiji la Rome kwa
ajili ya kulinunua.
Martin katika utetezi wake alidai kuwa, Balozi Mahalu
hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida
kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.
Akiongozwa na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma
zinazomkabili, Grace alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi
Mahalu mashtaka yote sita yanayomkabili hakuyatenda, aliwasilisha
mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali.”
Pia Martin alihoji sababu ya upande wa Jamhuri kutomleta
mmiliki wa jengo hilo la ubalozi kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea
kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo akidai walikwenda nchini humo
kufanya uchunguzi.