Afisa elimu ya sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Singida Voster Mgina akitoa taarifa ya kuungua kwa baadhi ya vitanda vya bweni la wasichana wa shule ya sekondari ya Wembere kata ya Mugungira tarafa ya Sepuka.
Moja ya vitanda vya  bweni la wasichana wa shule ya sekondari ya Wembere vilivyougua moto. (Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.

Bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya sekondari ya Wembere kata ya Mugungira tarafa ya Sepuka jimbo la Singida Magharibi limenusurika kuteketea kwa moto.

Mazingira ya kutokea kwa moto huo ambayo ni ya kutatanisha, inadaiwa kwa wakati huo wanafunzi 14 wa bweni hilo lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 46 hawakuwepo ndani ya bweni hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari wetu, Afisa elimu wa shule za sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Singida Voster Mgina, amesema moto huo uliweza kuzimwa na wanafunzi wakishirikiana na walimu wao kwa kutumia maji.

Amesema moto huo umeunguza vitanda viwili vya chuma aina ya  ‘double decker’, magodoro mawili na nguo za mwanafunzi mmoja.

Mgina amesema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na upelelezi zaidi unaendelea ili kujua chanzo cha moto huo.

Wakati huo huo, Mgina amesema hadi sasa shule hiyo yenye mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80, ni wanafunzi 22 tu wa kidato cha kwanza waliokwisha kuanza masomo shuleni hapo.

Kwa hisani ya MO BLOG