Na Mwandishi Maalum, AJAAT
MAWAZIRI wa Afya wa nchi za Afrika
walipokutana Mei 2009, mjini Addis Ababa, Ethiopia waliridhia suala la
kuzindua rasmi kampeni ya kuharakisha mchakato wa kupunguza vifo vya
wanawake vinavyotokana na uzazi na afya ya watoto katika nchi zao.
Kampeni
hiyo iitwayo CARMMA au Campaign for Accelerated Reduction of Maternal
Mortality In Africa ina malengo ya kuongeza kasi katika kupunguza vifo
vinavyotokana na uzazi na vya watoto wachanga, ili kufikia malengo ya
milenia namba 4, na 5, ifikapo mwaka 2015.
Kaulimbiu ya kampeni
hiyo, ‘No woman should die while giving life, Africa Cares’ ikiwa na
maana ya Afrika inajali: “Asife mwanamke wakati akileta kiumbe kipya.”
Baada
ya uzinduzi huo, kila nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika ilitakiwa
izindue kampeni yake katika nchi zao kwa lengo la kukabiliana na vifo
vinavyotokana na uzazi pamoja na watoto wachanga baada ya kuzaliwa.
Madhumuni
ya kampeni hiyo ni kuhamasisha jamii ichangie katika juhudi za
kitaifa za kuharakisha kupunguzwa kwa vifo vya wajawazito na watoto na
Tanzania ilizindua kampeni hiyo Juni 6, mwaka jana.
Katika
uzinduzi uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam ambao
ulifanywa na Waziri wa Afya na Usitawi wa Jamii, Dk Haji Mponda kwa
niaba ya Rais Jakaya Kikwete, kaulimbiu yake ilikuwa, “Tanzania inajali -
mwanamke asife kwa ajili ya kuleta kiumbe kipya; na mtoto asife kwa
sababu zinazozuilika.”
Kikwete alisema shughuli ya uzinduzi huo
ilikuja wakati mwafaka, kwani serikali ipo katika mchakato na inayo
mkakati mahususi wa afua, inayotekelezeka.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Dk. Alberic
Kacou, alisema kutotumika kikamilifu kwa vidonge vya uzazi wa mpango ni
sababu kubwa ya vifo vinavyotokana na uzazi Tanzania.
Dk. Kacou
akaishauri Serikali kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango
ili kudhibiti mimba zisizohitajika kwani tafiti zinaonyesha wanawake
wengi wanapenda kutumia mpango huo lakini hukosa huduma hizo.
“Wanawake
wengi wa Tanzania wanapenda kutumia dawa za uzazi wa mpango kwa ajili
ya kutoa nafasi kati ya watoto na wengine kudhibiti ukubwa wa familia,
lakini kwa bahati mbaya hawapati huduma hizo,” anasema Dk. Kacou na
kuongeza:
“Tumeweka lengo la kufikisha asilimia 60 kwa wanaotumia
uzazi wa mpango ifikapo mwaka 2015, lakini kwenye ripoti ya Tafiti ya
Demografia na Afya inaonyesha hatujafika hata nusu ya makadirio hayo ya
mwaka 2015”.
Utafiti wa Hali ya Maisha na Afya wa mwaka 2004/05
ulionyesha ni asilimia 47 ya wajawazito walijifungulia katika vituo vya
afya na utafiti kama huo mwaka 2010, umeonyesha ongezeko la kufikia hadi
asilimia 50.
Pamoja na mikakati hiyo, Tanzania imeanza kuona
mafanikio katika kupunguza vifo vitokanavyo na matatizo ya wazazi kutoka
wanawake 578 kwa kila vizazi hai 100,000, kama ilivyokuwa mwaka 2004,
hadi kuwa 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2011.
Mafanikio
hayo ni sawa na punguo la vifo 8,100 hadi 6,800 kila mwaka. Ili kufikia
Malengo ya Maendeleo ya Milenia, inabidi vipungue hadi view 193 kwa kila
mizao hai 100,000.
Vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka 5
vimepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka kumi iliyopita, kutoka vifo
147 kwa kila vizazi hai 1,000 kama ilivyokuwa mwaka 1999 hadi 81 kwa
kila vizazi hai 1000 mwaka ilipofikia mwaka 2010.
Punguzo hilo ni
la asilimia 45, ikilinganisha na ilivyokuwa mwaka 1999. Ili kufikia
lengo la milenia, vifo vya watoto wa umri wa chini ya miaka 5 vinatakiwa
kupungua hadi 54 kwa kila vizazi hai 1000.
Idadi ya vifo vya
watoto wa umri huo vimepungua kutoka 223,000 hadi 145,000 kwa mwaka na
vya watoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja vimepungua kwa asilimia 49
kutoka 99 kwa kila 1,000 kama ilivyokuwa 1999 hadi 51 kwa kila vizazi
hai 1,000 kufikia 2011.
Vifo vya watoto wachanga wenye umri wa
chini vya mwezi mmoja vimepungua kwa kiasi kidogo kwa zaidi ya nusu ya
walio chini ya mwaka mmoja, vikiwa ni 26 kwa kila vizazi hai 1,000.
Vingi vinatokana na matatizo, vikiwa ya uzazi.
Mwaka 2008, Rais
Kikwete alizindua Mpango kabambe wa kuongeza juhudi za kupunguza vifo
vya wajawazito na watoto (Road Map 2009-2015), ili kuhakikisha
tunakuwapo muongozo wa utekelezaji.
Hivyo, Serikali imechukua
hatua za kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za afya, kwa kuongeza
idadi ya vijana wanaodahiliwa kuingia vyuo vya afya na kufungua vyuo
vipya.
Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, wanafunzi
waliodahiliwa kuingia katika vyuo hivyo iliongezeka mara nne, kutoka
1,013, mwaka hadi 2007, kufikia 6,713 mwaka 2010, lengo likiwa kufikia
udahili wa wanafunzi 10,000 kwa mwaka, ifikiapo 2015.
Makala haya yameandaliwa na muungano wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayotetea kuboreshwa kwa huduma za uzazi wa mpango.