Licha
ya Serikali kuliarifu Bunge la Tanzania kuwa wanafunzi wote waliofaulu
darasa la saba mwaka 2011 kutoka mikoa 12 tayari wamejiunga na kidato
cha kwanza, imebainika bado kuna wanafunzi wameshindwa kujiunga na shule
kutokana na kipato duni cha familia zao.
Mmoja
wa wanafunzi hao Mwenjuma Magalu aliyechaguliwa kujiunga na Shule ya
Sekondari Komnyang’anyo wilayani Handeni ni miongoni mwa wanafunzi
walioshindwa kujiunga na sekondari kutokana na mama yake kushindwa
kumgharamia mahitaji ya shule.
Akizungumza
hivi karibuni kijijini Msasa, wilayani Handeni katika utafiti
uliofanyika kwa ushirikiano na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA),
mama wa mtoto huyo Hadija Magalu aliyetelekezwa na mumewe kwa muda mrefu
amesema ameshindwa kumsomesha mwanaye kutokana na kipato duni
alichonacho.
Magalu
amesema alipata taarifa za kufaulu kwa mwanae tangu Desemba 12, 2011 na
kuanza kujikusanya taratibu lakini hadi muda wa kwenda shule ulipofika
(Januari 9, 2012) alikuwa hajakamilisha baadhi ya vifaa vinavyohitajika
shuleni vikiwemo fedha ya ada na michango mingine.
Michango
iliyomkwamisha mwanafunzi Mwenjuma Magalu kujiunga na kidato cha kwanza
ni ada ya sh. 20,000, fedha ya taaluma sh. 10,000, fedha ya madawati
15,000, fedha ya sweta sh.10,000, kitambulisho sh. 5,000, ulinzi sh.
5,000, tahadhari 5,000 pamoja na fedha kwa ajili ya nembo ya shule sh.
2,000.
Akihutubia
Mkutano wa Saba wa Bunge la Tanzania lililomalizika hivi karibuni,
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda alisema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
kutoka mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara,
Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma na Tanga,
wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba wamefanikiwa kujiunga na Kidato
cha Kwanza.
Hata
hivyo mwanafunzi Magalu kwa sasa anafanya vibarua kwa moja ya kampuni
za Kichina zinazofanya ujenzi wa barabara inayopita Kijiji cha Msasa,
kwa madai anatafuta fedha za ada na endapo akikamilisha atahakikisha
anaendelea na elimu ya sekondari hapo baadae.
Mwandishi
wa habari hizi alipojaribu kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Handeni Hassan Mwachibuzi alisema ofisi yake haina taarifa za mtoto huyo
kushindwa kujiunga na shule, hivyo kumshauri mwandishi amueleze mtoto
huyo kufika ofisi za halmashauri ili aweze kujieleza na ikiwezekana
kusaidiwa.
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).