MAKETE
Wananchi wilayani Makete wameilalamikia sekta ya afya wilayani Makete kwa kitendo cha kutoondolewa takataka zilizolundikwa katika eneo la soko la wakulima Makete mjini, Mabehewani na Kona hali inayopelekea taka hizo kutoa harufu mbaya
Wananchi hao wamesema taka hizo zimekuwa nyingi lakini wahusika hawatoi taka hizo hasa eneo la sokoni kwani wameongeza uwepo wa taka hizo kunaweza kupelekea hatari ya kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, na kumtaka Bwana Afya wa wilaya kushughulikia tatizo hilo kwa haraka ili kuinusuru hali hiyo
Akizungumzia suala hilo Afisa Afya wa wilaya ya Makete Bw. Boniface Sanga amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema walikuwa wakitafuta eneo la kupeleka taka hizo nab ado halijapatikana lakini hivi sasa wanalazimika kuziondoa taka hizo haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya wakazi wa maeneo hayo wakiwemo watoto wanaocheza zilipo taka hizo
Bw. Sanga amewataka wafanyabiashara wa maeneo hayo pamoja na wakazi wa maeneo jirani wawe na vyombo maalum vya kuhifadhia kwa muda na sio kutupa taka hovyo mitaani, kwani kutupa taka hovyo ni kosa na yeyote atakayebainika atalipa faini kulingana na sheria inavyosema
Na Anitha Sanga na Obeth Ngajilo