MAKETE
Wajumbe wa kamati ya kudhibiti Ukimwi wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamefanya ziara ya siku mbili wilayani Makete kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali za kuzuia maambukizi mapya ya vvu na Ukimwi zinazofanywa na wilaya ya Makete
Katika ziara hiyo iliyojumuisha viongozi mbalimbali kutoka wilaya ya Korogwe akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mh. Kallaghe Yusuph, pia ameambatana na baadhi ya madiwani, wawakilishi wa watu waishio na VVU, Maafisa wa Serikali pamoja na Viongozi wa Dini.
Mh. Kallaghe ametoa pongezi kwa wadau pamoja na Serikali ya Makete kwa hatua ambayo wamefikia katika mapambano ya Ugonjwa wa ukimwi ambao kwa sasa unaendelea kupungua kwa kasi kubwa wilayani Makete ukilinganisha na miaka michache iliyopita ambapo Makete ilikuwa katika kiwango cha juu cha maambukizi ya vvu ukilinganisha na wilaya zingine hapa nchini.
Katika hatua nyingine wanakamati hao wametembelea baadhi ya vijiji vikiwemo Ivalalila kilichopo katika kata ya Iwawa pamoja na Kijiji cha Iniho kilichopo katani Iniho ambako waliweza kufanya mazungumzo na wananchi wa vijiji hivyo ili kujifunza zaidi namna wanavyojikinga na maambukizi mapya ya vvu, ambapo walijifunza namna waviu wanavyotoa elimu kwa watu mbalimbali kupitia vikundi vyao
Wajumbe hao waametoa shukrani kwa ushirikiano walioupata kutoka kwa viongozi wa Halmashauri kwa Kufanikisha zoezi la kujufunza na kubadilishana uzoefu na namna walivyoweza kupambana na maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi Wilayani Makete.
Na Aldo Sanga.