TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA IRINGA MHE. DR. CHRISTINE G. ISHENGOMA (MB.) KWA VYOMBO VYA HABARI, VIONGOZI WA DINI, WAZEE MASHUHURI NA VYOMBO VYA USALAMA KUHUSU UHAMASISHAJI WA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA ZOEZI LA SENSA YA WATU NA MAKAZI TAREHE 27 APRILI, 2012.

Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 26 Agosti 2012 na kuendelea kwa takriban siku saba. Hii itakuwa Sensa ya tano (5) tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. 

Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na kufuatiwa na Sensa nyingine za mwaka 1978, 1988 na 2002.

Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, Sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. 

Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwani mbali ya kutimiza malengo ya kawaida ya sensa, takwimu zitakazokusanywa katika sensa hiyo zitatumika katika kutathmini utekelezaji wa mipango yetu mikubwa ya maendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi kilichopita.

Mipango hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania - MKUKUTA kwa Tanzania bara  Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar - MKUZA kwa upande wa Zanzibar. Halikadhalika, takwimu za Sensa ya mwaka 2012 zitatumika kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Milenia 2015.





Nafasi zenu  katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi
Hamna budi kufahamu kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Kwa hiyo mnapaswa kuwahamasisha wananchi ili wahesabiwe  na wahesabiwa mara moja tu, ili takwimu zitakazokusanywa ziwe sahihi na za uhakika. Usahihi wa takwimu katika kila eneo ndio utimilifu wa takwimu za taifa.

Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuhamasisha wananchi: tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na yatakayojiri wakati wa zoezi la kuhesabu watu.  Jambo jingine la kuzingatia ni kuwepo kwa mawazo au hofu dhidi ya zoezi la Sensa. Ni muhimu sana kuwatoa hofu wananchi kwa kuwaelimisha kuwa zoezi la Sensa halihusiani kabisa na hofu au imani walizonazo.  Hamasa ifanyike hasa kwa wanawake, wanaume, vijana, watoto na watu wenye ulemavu.

Ningependa muwahakikishie wananchi kuwa taarifa watakazozitoa wakati wa Sensa zitakuwa siri na zitatumika kwa masuala ya kitakwimu pekee.  

Nawasihi ndugu wananchi mtekeleze jambo hili.
 SENSA KWA MAENDELEO: JIANDAE KUHESABIWA


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo