Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mountain Chafukwe wilayani Makete wamesema kukamilika kwa bweni la wasichana shuleni hapo ni kichocheo cha kupanda kwa taaluma kwa wasichana shuleni hapo
Hayo yamebainika kufuatia mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kwa kushirikiana na jamii wamejenga bweni shuleni hapo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike wapatao 48
Kwa nyakati tofauti baadhi ya wasichana wanaolala kwenye bweni hilo walishukuru kukamilika kwa ujenzi wa bweni hilo kwani imewasaidia wao kuishi shuleni hapo hali iliyowasaidia kuongeza muda wa kujisomea na kuepukana na vishawishi walivyokuwa wakivipata mtaani kutokana na kupanga mitaani
Mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe redioni amesema wanafunzi kupanga mitaani kuna madhara makubwa hasa kujikuta wakishawishika kufanya ngono na watu mbalimbali
“Unajua sisi wasichana tuna matatizo mengi sana yaani vishawishi ni vingi sana kwetu hasa nyakati za usiku, tunajikuta tukishawishika kufanya ngono tukiwa huko mitaani lakini kwa sasa bweni hili limetupunguzia matatizo hayo sana tuu”alisema msichana huyo
Aliongeza kuwa “ninachukizwa sana na tabia za baadhi ya vijana waendesha pikipiki maarufui kama bodaboda kwani ni wasumbufu mara wakutanie kwanini unatembea kwa miguu, njoo nikupeleke uendako, au ukiwa na shida ya fedha unione kumbe lengo lao ni kutaka kufanya mapenzi hakuna kingine”
Pamoja na kukamilisha ujenzi wa bweni hilo mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF wamefanikiwa kutengeneza vitanda pamoja na magodoro yanayotosheleza malazi kwa wanafunzi wote 48
Kwa upande wake mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo Wema Kihombo alisema ameongeza masaa ya kujisomea lengo likiwa ni kufaulu na kuendelea na masomo hadi chuo kikuu kwa mazingira ya shule yanaruhusu
Naye mkuu wa shule hiyo Veronica Kiwope aliishukuru serikali kupitia TASAF kwa kuweza kukamilisha ujenzi wa bweni la wasichana shuleni hapo na kutoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo kuwapeleka watoto wao wa kike kuishi bwenini
“Kuna baadhi ya wazazi hawaoni umuhimu wa watoto wao kulala bwenini kwa sababu ya kuhofia kuwa gharama yake ni kubwa, nimnawaomba wazazi tushirikiane ili tuwakomboe watoto wa kike”alisisitiza Mwalimu Kiwope
Shule ya sekondari ya Mout Chafukwe ambayo ipo kandokando mwa barabara kuu ya Iringa- Mbeya kwenye kijiji cha Mfumbi kata ya Mfumbi wilayani Makete katika mkoa mpya wa Njombe ina mikakati ya kuinua kiwango cha elimu shuleni hapo ikiwemo wanafunzi wote wa kike na wa kiume kuishi shuleni hapo