Kikundi cha kina mama wajane kilichopo katika kijiji cha Kitula kata ya Kipagalo wilayani Makete kimesema kimeanza kupata matunda ya mradi wao wa ufugaji wa nguruwe wa kisasa
Kikundi hicho chenye wanachama kumi na mmoja kilipata mradi wa ufugaji wa nguruwe kutoka kwenye mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF ambapo walipewa jumla ya nguruwe majike 12 na dume mmoja
Mbali na nguruwe hao pia walipewa mbuzi 12 hivyo kuwanufaisha wanakikundi hao kwa kila mmoja kupata nguruwe mmoja jike na mbuzi mmoja
Afisa kilimo na mifugo wa kata ya Kipagalo Hebren Mahava aliyataja mafanikio ambayo yamepatikana kupitia kikundi hicho kuwa nguruwe 11 wameshazaa watoto 67 kati ya hao majike ni 33 na madume 34 na tayari watoto hao wote wa nguruwe wamepata wanunuzi ambapo kila mmoja atauzwa kwa shilingi elfu thelathini
Alisema kuwa siri ya mafanikio hayo ni kuandaa mahitaji yote muhimu wakati wa kuibua mradi huo kama vile dawa, vyakula vya madini, pumba na pampu kwa ajili ya kupulizia dawa za kuua wadudu wasababishao magonjwa kwa nguruwe na pia wafugaji hao wamepewa mafunzo maalum ya utunzaji na ufugaji bora wa nguruwe
Naye Lydia Chaula ambaye ni mwanakikundi aliushukuru mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kwa kuweza kuwapa mradi huo kwani imempunguzia ukali wa maisha uliokuwa unamkabili kutokana na ujane wake ikiwemo kuitunza familia yake aliyoachiwa na marehemu mume wake
“Ninamshukuru Mungu kwani nguruwe wangu amezaa watoto 07 na wote wamepata wateja hivyo nimeshapata fedha kwa ajili ya kulipa ada na mahitaji mengine ya shule kwa mwanangu anayesoma kidato cha tatu hivi sasa”alisema Chaula
Mbali na faida ya kuuza watoto hao wa nguruwe mama huyo mwenye watoto watatu alisema anapata mbolea ya kutosha kwa ajili ya kupandia mazao
Mradi huo utakuwa endelevu kwani moja ya kanuni iliyowekwa na wanakikundi ni kutokuuza nguruwe ama mbuzi bila idhini ya kikundi na iwapo atauza lazima anunue nguruwe mwingine ili aendelee kumfuga