Madaktari wasitisha mgomo warudi kazini |
Sunday, 11 March 2012 10:46 |
![]() CHAMA cha Madaktari Tanzania (Mat) kimetangaza kusitisha mgomo wa nchi nzima kuanzia jana mchana, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kumheshimu Rais Jakaya Kikwete, huku kikiwatangaza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya kuwa maadui namba moja wa sekta ya afya nchini. Uamuzi huo wa kurejea kazini umekuja siku nne tangu madaktari hao walipoanza mgomo kwa mara ya pili, wakishinikiza Serikali kutekeleza madai yao, likiwemo la Dk Mponda na Dk Nkya kujiuzulu. Februari 9 mwaka huu madaktari hao walirejea kazini baada ya kugoma kwa siku 17 wakishinikiza Serikali itekeleze madai yao kadhaa, likiwemo suala la nyongeza ya posho na kuwajibishwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Kurejea kwao kazini kulikuja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa. Taarifa ya viongozi wa MAT iliyotolewa mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa Donbosco jijini Dar es Salaam, walisema wamemsimamisha uanachama Dk Nkya kwa kipindi cha miaka miwili na kuongeza kuwa licha ya madaktari kurejea kazini, hawako tayari kufanya kazi chini ya uongozi wa mawaziri hao. Uamuzi kusitisha mgomo ulikuja baada ya viongozi wa Mat hicho na wale wa Jumuiya ya Madaktari kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, juzi kujadili mgogoro wao. Kabla ya kufikia uamuzi huo wa kusitisha mgomo wao ulioanza Jumatano iliyopita, kulikuwa na mvutano mkali kwenye kikao chao cha ndani kilichofanyika ukumbi wa Donbosco, kutokana na baadhi yao kuafiki kurejea kazini huku wengine wakitaka mgomo huo uendelee hadi hapo Dk Mponda na Dk Nkya watakapojiuzulu. Ufafanuzi wa Mat Rais wa Mat, Dk Namala Mkopi, alisema katika kikao chao na Rais Kikwete walimweleza jinsi mawaziri hao wasivyokuwa na uwezo wa kusimamia sekta nzima ya afya. “Tulimweleza Rais kila kitu na yeye ametuelewa. Pia tulibaini kuwa kuna taarifa za uongo alizokuwa akipelekewa na baadhi ya watu,” alisema Dk Mkopi. Alisema kuwa Rais Kikwete ameyapokea madai yao kwa uzito mkubwa na kuwaahidi kuwa atayashughulikia. “Kutokana na hali hiyo leo (jana) tumefanya kikao cha ndani na madaktari na kuwaeleza yaliyojiri katika kikao chetu cha jana (juzi) na Rais Kikwete na wamekubali kurejea kazini, hivyo kuanzia sasa tumerejea kazini kama awali,” alisema Mkopi. Alifafanua kuwa mgomo wao haukuwa mashindano baina yao na Serikali wala kuiumiza jamii, bali walikuwa wakitafuta suluhu ya kuboresha huduma za afya nchini na kwamba hatua waliyofikia sasa ni nzuri. “Madaktari wote waliokuwa katika mgomo warejee kazini, na hivi sasa kutakuwa na mawasiliano ya karibu ili kuwaeleza hatua zilizofikiwa katika suala zima la Serikali kutekeleza madai yetu, tuna imani na Rais na tunajua atatekeleza madai yetu,” alisema Dk Mkopi. Sharti kwa Rais Dk Mkopi alisema kuwa katika mkutanoh huo walimweleza wazi Rais Kikwete, kuwa madaktari hawako tayari kufanya kazi na mawaziri wa afya. Alisema kuwa Dk Mponda na naibu wake Dk Nkya ni maadui namba moja wa sekta ya afya na kwamba ili madai yao yaweze kutekelezwa na kufikia hatua wanayoitaka, mawaziri hao wanatakiwa wasiwepo tena katika wizara hiyo. “Hatuna imani na mawaziri hao hata kidogo na hatuwezi kufanya kazi nao na katika kikao chetu, madaktari wote wamekubaliana hivyo,” alisema Mkopi. Alipoulizwa kama wamempa rais muda wa kutekeleze madai yao, alisema hawakumpangia, wala rais hakuwaeleza suala hilo atalishughulikia kwa kipindi gani, isipokuwa watakuwa wakipeana taarifa ya kila kitu kitakachokuwa kikiendelea. Dk Nkya asimamishwa Mat Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Rodrick Kabangila alisema kuwa MAT kimemsimamisha uanachama Dk Nkya kwa muda wa miaka miwili. “Kwa kipindi cha miaka miwili hatakuwa mwanachama hai wa Mat, tumeamua kumsimamisha uanachama kwa kuwa pamoja na mambo mengine, hatuna imani naye,” alisema Dk Kabangila. Kabla ya maamuzi Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari madaktari hao walikuwa na kikao cha ndani ambacho waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria. Habari za ndani kutoka katika kikao hicho kilichoanza saa 4:50 asubuhi na kumalizika saa 6:53 mchana, zinaeleza kuwa madaktari hao walivutana kuhusu mgomo, ambapo baadhi yao walitaka uendelee huku wengine wakitaka usitishwe kuokoa maisha ya watu wanaokufa bila hatia. Taarifa zinaeleza kuwa asilimia kubwa ya madaktari hao ilionyesha kuwa na imani na Rais Kikwete hali iliyowafanya wakubaliane kwa urahisi. Kauli ya Dk Mponda Gazeti hili lilipomtafuta Dk Mponda jana kwa simu, muda mfupi baada ya madaktari hao kusitisha mgomo wao; alisema kuwa hana la kuzngumza. “Katika hilo sina maoni yoyote na wala siwezi kusema kitu chochote,” alisema Dk Mponda na kukata simu. Rais alivyoingilia kati Juzi Rais Kikwete aliahirisha kulihutubia Taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, badala yake akaitisha mkutano wa faragha na viongozi wa MAT. Rais Kikwete alifanya kikao hicho juzi mchana Ikulu jijini Dar es Salaam, huku kukiwa na amri ya Mahakama ya Kazi inayowaamuru madaktari hao kurejea kazini kutokana na kesi iliyofunguliwa na Mwanasheria wa Serikali. Mpaka madaktari hao wanakwenda kuonana na Rais Kikwete, walikuwa katika mgomo kwa maelezo kuwa hawana taarifa rasmi ya Mahakama. Kikao cha juzi kilikuwa cha kwanza kwa Rais Kikwete kukutana na madaktari hao ambao kwa sasa wanagoma kwa mara ya pili. Baada ya kikao chao na rais, madaktari walitoka Ikulu bila kuzungumzia chochote. Katibu Mkuu wa Mat, Dk Kabangila alikataa kata kata kuzungumzia kilichoazimiwa kwenye mkutano huo na Rais Kikwete akasisitiza kuwa ataweka mambo hadharani siku inayofuata (jana). Hali ilivyokuwa hospitali Dar Ibrahim Yamola na Aidan Mhando wanaripoti kuwa kuanzia jana mchana huduma katika hospitali hizo, zilirejea katika hali ya kawaida baada ya madaktari kurejea kazini. Katika hospitali za Mwananyamala, Amana na Temeke huduma zilikuwa zinatolewa ingawa kulikuwa na idadi ndogo ya wagonjwa kama ilivyo kawaida yake. “Nimefika kumleta mwanangu anaumwa malaria na nimetibiwa kama kawaida nafikiri mgomo wao umemalizika,” alisema Mohamed Yasin mkazi wa Kinondoni aliyekuwa katika hospitali ya Mwananyamala. Chanzo cha mgogoro Januari 23 mwaka huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka alitangaza mgomo wa madaktari nchi nzima lengo likiwa kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao. Joto lilipanda zaidi baada ya kufukuzwa kwa madaktari waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika hosptali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambapo Mwenyekiti wa Mat, Deogratus, alisema wapo 225 huku Serikali kwa upande wake ikidai walikuwa 197. Sorce:Mwananchi |