WAGANGA WA JADI WATAMBULIWA

MAKETE                     
Mkutano wa utambuzi wa Waganga wa jadi na Tiba asili umefanyika  katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Makete kwa lengo la kuwapata waganga wa jadi wanaotoa tiba za kweli kwa watu na si matapeli

Akizungumza na Waganga na Wakunga hao wa Jadi Katibu wa Kamati tendaji ya kutambua waganga wa jadi Mkoa wa Iringa Bw. Maiko Kalinga amesema ni marufuku kwa mganga yeyote wa jadi kupiga ramli kuanzia hii leo.

Ameongeza kuwa kumekuwa na tabia ya wakunga wa jadi kuwapa dawa za asili za uchungu kwa kina mama wajawazito pamoja na kutoa mamba jambo ambalo amelikemea vikali na kuliita kuwa ni sawa na mauaji hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao

Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Makete (OCS) Peter Kaiza amewataka waganga hao wa jadi kufanya shughuli zao za kutibu matatizo ya watu na sii kuchangia kuwepo kwa mauaji ya watu kutokana na imani za kishirikina.

Amesema waganga wamekuwa wakiwaambia wateja wao kuwa ili wafanikiwe wanatakiwa waje na viungo vya watu mfano wazee, jambo ambalo amelikemea na kuliita kuwa ni uuaji na sheria haitawaacha waganga wa aina hiyo

Naye Katibu wa Chama Cha Waganga wa jadi na Wakunga mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Kamati tendaji Dr. Joseph Mkolwe amesema zoezi hilo litasaidia kutambua Waganga wa kweli ambao wanatoa huduma ya kweli kwa jamii na kuepuka matapeli ambao wanatoa sifa mbaya kwa Waganga wote waliopo nchini.


Mwakilishi kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wilaya ya Makete Bw. Felician Chawala ameshukuru kwa zoezi hilo ambapo amesema Waganga wa Jadi, Waakunga wa Jadi pamoja na Waganga wa hospitali wote lengo lao ni kutoa huduma za kuwaponya watu na si kusababisha watu kupoteza maisha yao hivyo wanatakiwa kufanya kazi yao kiukweli.

Aidha mwenyekiti wa Waganga wa jadi wilaya ya Makete Bw. Meja Sanga almaarufu kama “Mwakipande” amesema wilaya ya makete ina waganga zaidi ya 200 lakini huwa hawajitokezi pindi wanapoitwa kwa ajili ya kupewa mafunzo au semina mbalimbali, na kuwataka waganga wote kujitokeza pindi wanapohitajika

Katika hatua isiyo ya kawaida Waganga wa jadi wapatao sita wameamua kuacha shughuli zao za uganga na kuamua kufanya shughuli nyingine.

Waganga hao ni Adamu Lutindi Exavery Lihogo wote wakazi wa kijiji cha Kigala Ikuwo, Teleza Sanga wa kijiji cha Ugabwa Lupalilo, Josephat Mbalila, Matamshi Fungo wote wakaazi wa Ipelele na Jabil Mgeni wa Lupombwe Mbalache

Wamesema wameamua kuachana na kazi hiyo ya Uganga kutokana na masharti ya usajili yaliyowekwa na serikali kwa sasa ambapo wamesema ni magumu na pia hawana fedha za kulipia fomu hizo huku wengine wakisema wameamua kuacha wao wenyewe kutoka moyoni.

Na. Edwin Moshi











JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo